Thursday, November 2, 2017

TIGO YAMKABIDHI KOMPYUTA MBUNGE WA JIMBO LA ILEMELA

 Mwandishi wetu ni Yusuph Ludimo
Kampuni ya Huduma za Simu za mkononi nchini ya TIGO leo imemkabidhi Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula jumla ya Kompyuta 11 kwaajili ya Zahanati na Vituo vyote vya Afya vinavyopatikana ndani ya wilaya ya Ilemela ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, ukusanyaji wa mapato na utunzaji wa kumbukumbu

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kuishukuru Kampuni ya Tigo kwa jitihada zake za kuunga mkono Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe Rais Dkt John Magufuli  katika kutoa huduma stahiki kwa jamii ili kujiletea maendeleo  pia ametaka kutunzwa na kuhakikisha Kompyuta hizo zinafanya Kazi iliyokusudiwa

"Kompyuta hizi zitaenda kutusaidia katika kipindi hiki ambacho Serikali inahama katika ule mfumo wa kawaida wa kukusanya mapato  kwa zile risiti za kawaida ambazo tumezoea na kuingia katika utaratibu wa mifumo ya kielektroniki , Lengo la Serikali ni kuona kwamba ile mianya yote ya ubadhirifu wa mapato inazibwa " Alisema


Aidha Mhe Dkt Angeline Mabula amevitaja Vituo vya Afya na Zahanati zitakazonufaika na Kompyuta hizo kuwa ni kituo cha afya cha Buzuruga, Karume, Sangabuye, Zahanati ya Nyamhongolo, Nyakato,Nyerere, Pasiansi, Ilemela, Kiloleli, Kirumba na Shibula huku akiahidi kuwa huu ni mwanzo vituo vyengine na ofisi za kata vitafuata kadri ya fursa zitakapokuwa zinajitokeza

 Akimkaribisha Mbunge huyo Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga akiwa na mkurugenzi wa manispaa yake John Wanga na mwenyekiti wa kamati ya huduma Mhe Sarah Ng’wani amemshukuru Mhe Mbunge kwa jitihada anazozichukua ili kuleta maendeleo huku akiahidi ushirikiano na usimamizi wa Kompyuta hizo ili ziweze kufanya kazi na kutimiza  malengo yaliyokusudiwa

Nae Meneja wa Tigo Kanda ya Ziwa Ndugu Edger Mapande aliyeambatana na Meneja wa Tigo Mkoa wa Mwanza Bwana Kassim Aziz mbali na kutambulisha Kampeni mpya ya Tigo iliyobebwa na jina la TUMEKUSOMAA..! amesema kuwa Kampuni yake itaendelea kutambua mahitaji ya jamii na kuyatafutia ufumbuzi kama ilivyofanya kwa Jimbo la Ilemela na imekuwa ikifanya hivyo hata katika maeneo mengine nchini kwa makundi tofauti tofauti ya Jamii kulingana na uhitaji

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga ’

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
02.11.2017







 

No comments:

Post a Comment