Tuesday, August 6, 2019

SERIKALI YAFUTA KODI ZA ARDHI KWA MAENEO YA KUABUDIA

Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Magufuli imefuta kodi ya ardhi kwa maeneo yasiyozalisha na kutumika kwaajili ya ibada kwa kigezo cha taasisi husika kuomba msamaha huo kwa kufuata maelekezo yaliyoko katika tangazo la Serikali GN 347.

Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizindua mikutano ya kiroho maarufu kama makambi au vibanda kwa kanisa la WaAdventista Wasabato katika kanisa la Pasiansi jijini Mwanza ambapo hufanyika mara moja kila mwaka ndani ya mwezi wa sita mpaka wa tisa, Akisema kuwa Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na itaendelea kutatua kero mbalimbali zinazokabili taasisi za dini ili kujenga jamii sawa na yenye hofu na Mungu kuruhusu shughuli za kimaendeleo ziweze kutekelezeka kwa urahisi pamoja na kupongeza taasisi za dini kwa kutekeleza miradi mikubwa yenye manufaa kwa jamii kama hospitali ya Sabato Pasiansi iliyojengwa na kanisa hilo inayohudumia watu wote bila kujali tofauti za imani za kidini

‘.. Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na kama ilivyojinasibu yenyewe ni Serikali ya wanyonge, Imefuta kodi za ardhi kwa maeneo ya kuabudia ili mradi ufuate taratibu zinazotakiwa, Na kulifanya hili kwa urahisi baba askofu unaweza kutafuta gazeti la Serikali namba 347 ..’ Alisema 

Aidha ameongeza kuwa Serikali inaendelea na utatuzi wa migogoro mbalimbali ya Ardhi nchini ikiwemo ile inayohusu taasisi za kidini huku akiwaomba kuendelea kumuombea Mhe Rais Dkt John Magufuli na nchi kwa ujumla wake kufuatia kazi kubwa ya kuiletea nchi maendeleo ikiwemo ujenzi wa miradi mikubwa ya ufuaji wa umeme maarufu kama striggers gorge, ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa miundombinu ya barabara, utoaji wa elimu bila malipo na uboreshaji wa sekta ya afya kwa kujenga hospitali za wilaya, vituo vya afya, zahanati  na utoaji dawa.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Nyanza Kusini, Sadock Butoke amemshukuru mbunge huyo na kumhakikishia kuwa kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi pamoja na kumuomba kuendelea na jitihada za kutatua migogoro ya ardhi inayokabili kanisa hilo na wananchi wengine sanjari kuruhusiwa kulipa kwa awamu malimbikizo ya kodi ya zamani ya ardhi wanayodaiwa.

Katika sherehe hizo Dkt Mabula alikagua ujenzi wa hospitali ya kanisa Sabato Pasiansi pamoja na  kuzindua kanda kaseti ya pili ya Kwaya ya kanisa hilo.
















No comments:

Post a Comment