Tutaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo hata
maeneo ya wapinzani kwa sababu shughuli za maendeleo hazina chama wala
hazihitaji ubaguzi sisi wote lengo letu ni moja kujiletea maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mbunge wa Viti maalumu wa mkoa
wa Mwanza Mhe Kemilembe Lwota wakati akikabidhi vifaa vya kutolea huduma za
afya katika kituo cha afya Buzuruga kilichopo kata ya Buzuruga manispaa ya
Ilemela vikiwemo vitanda 10, magodoro 10 na mashuka 20 vyenye thamani ya
Jumla ya Shilingi Milioni Nane Laki Moja
na elfu Tisini na Tisa ambapo amesema kuwa Serikali ya chama cha mapinduzi chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli
itaendelea kuthamini afya za waTanzania
kwa kutekeleza miradi mikubwa ya afya ili kuhakikisha afya za wananchi
wake zinakuwa imara na nzuri bila kujali tofauti zao za kiitikadi za vyama vya
siasa ama nyenginezo
‘… Maendeleo hayana chama, maendeleo hayabagui ukiwa ccm,
ukiwa chadema ni lazima utatumia huduma zinazotolewa kituo hapa …’ Alisema
Aidha Mhe Kemilembe amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela
Mhe Dkt Angeline Mabula sambamba na kuwaomba wananchi wa jimbo hilo kuendelea
kumuunga mkono kwa jitihada kubwa
anazozifanya katika kuhakikisha anawatumikia wananchi wake na kuwaletea
maendeleo
Akimkaribisha Mbunge huyo wa Viti maalumu, Mbunge wa Jimbo
la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula mbali
na kushukuru, amempongeza Mhe Kemilembe kwa kuunga mkono jitihada za Mhe Rais
katika kuimarisha sekta hiyo ya afya huku akiwaasa wananchi wa Jimbo hilo
kuendelea kuchangia huduma za afya pamoja na kuanzisha miradi ya maendeleo
inayotekelezwa kwa utaratibu wa utatu kwa maana ya kuhusisha nguvu za wananchi,
nguvu za mbunge na nguvu za serikali kupitia halmashauri ya manispaa ya
Ilemela.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi, mtaalamu wa huduma za afya
ya uzazi na mtoto kwa manispaa ya Ilemela
Bi Nyabwire Lukumai mbali na kutaja changamoto zinazokabili kituo hicho
cha afya, ametaja zahanati zitakazonufaika na msaada huo wa vifaa vya kutolea
huduma za afya vilivyotolewa kuwa ni zahanati ya Nyamhongolo, zahanati ya
Ilemela, Zahanati ya Nyakato, Zahanati ya Kabusungu na Zahanati ya
Nyamwilolelwa.
Akihitimisha Diwani wa kata ya Buzuruga, Mhe Richard
Machemba ameshukuru kwa msaada huo huku akiwaomba wananchi kuendelea kumpa
ushirikiano mbunge wa jimbo hilo na mbunge huyo wa viti maalumu kwa namna
wanavyojitoa katika kutekeleza shughuli za kimaendeleo hasa katika kata yake
bila kujali tofauti za kiitikadi za kichama.
Makabidhiano hayo pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wa CCM ngazi ya wilaya na mkoa wakiongozwa na katibu wa CCM wilaya ya Ilemela
Achen Maulid na katibu wa UWT mkoa wa Mwanza.
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
14.12.2018
No comments:
Post a Comment