Wednesday, November 21, 2018

DKT ANGELINE MABULA: SERIKALI HAIHUSIKI NA FIDIA ZA URASIMISHAJI MAKAZI

Serikali haitahusika na fidia yeyote inayotokana na zoezi la urasimishaji wa makazi linaloendelea sehemu mbalimbali nchini na badala yake kamati za urasimishaji makazi za eneo husika kwa kushirikiana na  wananchi wake wanatakiwa kushughulikia changamoto zote zinazojitokeza katika zoezi hilo pamoja na kumfidia mwananchi atakaeathiriwa na zoezi hilo. 

Kauli hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Ilemela ambae pia ni naibu waziri wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kikazi jimboni humo juu ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi kwa kushirikiana na mkuu wa wilaya ya Ilemela, wakuu wa mashirika ya  umma ya TANESCO, TARURA na MWAUWASA, mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela na wataalamu wake katika kata ya Kitangiri, Pasiansi na Kirumba  ambapo amesema kuwa Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ni sikivu na ina lengo la kumkomboa mwananchi wa kawaida, Hivyo kuamua kuanzisha zoezi la urasimishaji wa makazi kwa nia ya kuwakomboa wananchi wake kiuchumi ili waweze kutumia ardhi waliyonayo kama mtaji na rasilimali muhimu katika kujiongezea kipato baada ya kuiongezea thamani kwa kupata hati miliki na kupimiwa huku akiwaasa kuhakikisha wanamaliza changamoto zote zinazotokana na zoezi hilo ikiwemo utoaji wa fidia kwa waathiriwa.

‘…Serikali yenu ni sikivu imeamua kuleta zoezi la urasimishaji wa makazi ili kuongeza thamani ya ardhi yenu, Lakini niwaambie Serikali haitahusika na fidia zinazotokana na zoezi hili ni wajibu wa wananchi na kamati zao za urasimishaji kuhakikisha wanamfidia yeyote atakaeathiriwa na zoezi hili …’ Alisema 

Aidha amewataka wananchi hao kumuombe na kumshukuru Mhe Rais Dkt John Magufuli kwa jitihada kubwa anazozifanya za kuiletea nchi maendeleo kupitia uchumi wa viwanda ikiwemo uanzishwaji wa miradi mikubwa ya reli ya kisasa, ununuzi wa ndege mpya, upanuzi wa uwanja wa ndege, uongezwaji wa bajeti ya wizara ya afya na utoaji wa elimu bure.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela,  Ndugu Amosy Zephania amesema kuwa manispaa yake itaendelea kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo ukarabati wa mwalo wa Mihama wa kata ya Kitangiri, ukarabati wa miundombinu ya shule na huduma za afya huku akiwataka kuhakikisha wanashirikiana na Serikali yao kujiletea maendeleo.

Nae mkuu wa wilaya hiyo Mhe Severine Lalika amewataka wananchi hao kuhakikisha wanakuwa mabolozi wazuri wa ulinzi na usalama wa raia na mali zao pamoja na kuzingatia sheria na taratibu ikiwemo kujenga kwa kufuata kibali cha ujenzi na sheria za mipango miji.

Akihitimisha ziara hiyo, Mwenyekiti wa umoja wa vijana taifa Comred Kheri James mbali na kumpongeza mbunge huyo kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi wake maendeleo amewaasa maafisa maendeleo ya jamii kuacha kukaa ofisini na badala yake kwenda kwa wananchi kusikiliza kero zao na  kuwaelimisha juu ya fursa za mikopo wanayoitoa kisheria.

'Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'

Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
21.11.2018













No comments:

Post a Comment