Tatizo la ukosefu wa umeme katika mitaa ya manispaa ya
Ilemela yenye sura ya kijiji kuwa historia ifikapo Januari, 2019.
Kauli hiyo imetolewa leo na meneja wa shirika la umeme
nchini (TANESCO) kwa kanda ya Ilemela mkoa wa Mwanza Mhandisi Ezekiel Simon
Mashola akijibu maswali ya wananchi wa Kata ya Shibula juu ya ukosefu wa Umeme
wa uhakika wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu
Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline
Mabula iliyofanyika katika mtaa wa Semba ili kusikiliza changamoto, kero na
ushauri kutoka kwa wananchi hao juu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
kimaendeleo jimboni humo ambapo amewahakikishia kuwa kabla ya Januari 31, 2018
maeneo yote ya jimbo hilo yatakuwa na umeme wa uhakika baada ya kupatikana kwa
vifaa vitakavyotumika kukamilisha mradi wa umeme vijijini (REA) kwa awamu ya
Tatu mzunguko wa kwanza mara baada ya
kusimama kwa mradi huo kufuatia kukosekana kwa vifaa
‘… Changamoto iliyokuwa inamkabili mkandarasi ilikuwa ni
vifaa ndio mana mkaona kama mradi umefifia hivi, Lakini hivi karibuni tulikuwa
na kikao na mkandarasi wa REA, Mkurugenzi wa REA na baadae Waziri wa nishati
pale Dodoma, Transifoma zishafika, nguzo zipo, mita zimefika tunachosubiria ni
utekelezaji tu …’ Alisema
Aidha Mhandisi Ezekiele ameongeza kuwa jumla ya mitaa 7 ya
Buganda, Semba, Lwashi, Iponyabugali, Igalagala, Kabusungu na Lutongo
itanufaika na huduma hiyo kwa 100% huku mitaa itakayosalia ikipangwa katika
awamu ya tatu mzunguko wa pili unaotaraji kuanza hivi karibuni.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline
Mabula mbali na kumshukuru Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa utekelezaji wa miradi
ya maendeleo, kuwasisitiza vijana kutumia fursa za upatikanaji wa mikopo na
elimu ya ujasiriamali ili kijikwamua kiuchumi, amesema kuwa mpaka sasa 89% ya ahadi zake alizozitoa wakati akiomba kura
kwa wananchi amekwisha zitekeleza ikiwemo kuboresha miundombinu ya Elimu ambapo
vyumba vya madarasa vimejengwa kupitia mradi wa ufatuaji matofali chini ya
taasisi ya The Angeline Foundation, kuboresha mazingira katika vituo vya afya
na zahanati ambapo zahanati mpya zimezidi kujengwa ikiwemo ile ya Buganda,
Lukobe na Nyamhongolo sambamba na kuzipandisha hadhi zile za zamani kuwa vituo
vya afya huku jengo la dharula la hospitali ya wilaya likikamilika kwa zaidi ya
90%, kuanzisha mashindano mbalimbali ya michezo ambapo mashindano ya Angeline
Ilemela Jimbo Cup yamekuwa yakifanyika kwa lengo la kuibua vipaji vipya na
kuviendeleza vile vya zamani, kusogeza huduma ya maji kwa wananchi ambapo mbali
na shirika la maji safi na maji taka MWAUWASA kutekeleza miradi mbalimbali
mbunge kwa kushirikiana na wadau wameweza kujenga visima katika maeneo tofauti
tofauti kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Nae Diwani wa kata hiyo, Mhe Dede Swila kwa niaba ya
wananchi wa kata hiyo amemshukuru mbunge huyo kwa kazi kubwa anayoifanya katika
kuwaletea maendeleo huku akiahidi ushirikiano, Sanjari na kuwaomba wazee wa
kata hiyo kuacha mambo ya kishirikina ili watumishi wa umma waliopo katika kata
yao waweze kufanya shughuli zao kwa weredi.
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
15.12.2018.
No comments:
Post a Comment