Wananchi wa Jimbo la Ilemela wametakiwa kuendelea kumuunga
mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Joseph Pombe
Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo anayoifanya.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt
Angeline Mabula wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Bugogwa katika
viwanja vya Kabangaja ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kusikiliza kero za
wananchi, changamoto na ushauri zinazowakabili ili kujiletea maendeleo, Mhe Dkt
Angeline Mabula amewataka wananchi hao kumshukuru na kuendelea kumuunga mkono
Rais Magufuli kwa mageuzi makubwa anayoendelea kuyafanya ili kufikia uchumi wa
kati kupitia sera ya viwanda ambapo miradi mikubwa ya kimaendeleo imeendelea
kutekelezwa ikiwemo ununuzi wa ndege za kisasa, ujenzi wa reli ya kisasa(SGR),
uboreshaji wa sekta ya afya na kuongeza bajeti ya sekta hiyo, ujenzi wa mradi
wa ufuaji wa umeme(Striggers Gauge), upanuzi wa viwanja vya ndege na ujenzi wa
miundombinu ya barabara na madaraja pamoja na kutoa elimu bure kwa shule za
msingi na sekondari hadi kidato cha nne.
‘… Tuna Rais anaejali watu wake hasa wale wanyonge, amefuta
shuru na tozo zote zilizokuwa kero, ameamua kutoa vitambulisho kwa
wafanyabiashara wadogo wenye mtaji wa chini ya milioni 4 ambao hawapo kwenye
mfumo wa mamlaka ya ukusanyaji kodi (TRA) ili waweze kukua kiuchumi, Mungu
atupe nini ndugu zangu zaidi ya kumuombea na kuendelea kumuunga mkono …’
Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amekemea kitendo cha kutwaa ardhi za
wananchi bila kulipa fidia kama taratibu na sheria za ardhi na mipango miji
zitakuwa zimefuatwa huku akiwaasa wananchi hao kuhakikisha wanalipa gharama za
urasimishaji makazi na kuhakikisha wanachukua hati ili kuongeza thamani ya
maeneo yao sanjari na kuwaasa wafanya biashara wakubwa kuacha kudanganya ili
waweze kunufaika na vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo vilivyotolewa na
Mhe Rais.
Kwa upande wake afisa ardhi wa manispaa ya Ilemela, Ndugu
Shukran Kyando amesema kuwa mpaka itakapofika Januari, 2019 wananchi wa mitaa
ya Nyafula, Lugeye na Sangabuye waliokuwa katika mradi wa upimaji wa ardhi na
makazi kwa awamu ya kwanza watakuwa wamelipwa fidia huku akiwaasa kuwa
wavumilivu na kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalamu ili kumaliza salama
zoezi hilo.
Akifunga mkutano huo Mwenyekiti wa Mtaa wa Kabangaja, Ndugu
Sebastian Lukona amemuomba Mbunge wa Jimbo hilo kufikisha salamu wa wananchi wa
mtaa wake kwa Rais Mhe Dkt John Magufuli na kuongeza kuwa wananchi wake
wanaunga mkono kazi kubwa ya kuleta maendeleo anayoifanya na kuahidi kuendelea
kumuunga mkono.
Ziara ya mbunge Mhe Dkt Angeline Mabula pia ilihudhuriwa na
wataalamu wa manispaa ya Ilemela, shirika la maji MWAUWASA, wakala wa barabara
TARURA, shirika la umeme TANESCO, na Madiwani wa kata za Sangabuye, Bugogwa na
Shibula.
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
17.12.2018.
No comments:
Post a Comment