Jeshi la magereza mkoa wa Mwanza limempongeza na kumshukuru
mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa msaada wa matofali
aliyoyatoa na kutumika katika ujenzi wa jiko na stoo kwa gereza la wanawake
Butimba.
Kauli hiyo ya pongezi iliyoambatana na cheti cha shukrani
imetolewa leo na mwakilishi wa mkuu wa gereza la Butimba Afande SSP Edith
Edward Mbogo wakati wa mkutano wa mbunge
wa jimbo hilo na wananchi wa mtaa wa Ilalila kata ya Shibula ikiwa ni mwendelezo
wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi, changamoto na ushauri juu ya
miradi midogo na mikubwa inayotekelezwa katika eneo lao na nchi kwa ujumla wake
ambapo amesema kuwa jeshi la magereza linatambua na kuthamini juhudi kubwa
zinazofanywa na Mhe Dkt Angeline Mabula katika kuwaletea wananchi maendeleo na
jeshi likiwa sehemu ya jamii litaendelea kuunga mkono juhudi hizo
‘… Jeshi la magereza linatambua juhudi unazozifanya kwa
wananchi na Sisi ni sehemu ya wananchi wako, Tunatambua namna unavyotusaidia
naomba nichukue fursa hii kukukabidhi zawadi ndogo tuliyoiandaa kwa sababu
Angeline Foundation ilitusaidia matofali ya kujenga jiko na stoo kwa gereza la
wanawake Butimba …’ Alisema
Aidha Afande Mbogo amewatoa hofu wananchi wa mtaa wa Ilalila
kuwa jeshi la magereza limekwishafanya uhakiki wa awali wa eneo la mtaa huo
wanalotegemea kulitwaa kwaajili ya ujenzi wa gereza la wilaya ya Ilemela hivyo
kuwataka kuendelea kuwa wavumilivu kusubiri hatua zitakazofuata ili baadae
waweze kulipwa fidia.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline
Mabula ameshukuru Jeshi hilo kwa kutambua na kuthamini mchango wake huku akiahidi kuendelea kushirikiana nao
kuhakikisha wanawaletea wananchi maendeleo sambamba na kuwaomba kufikisha
salamu zake kwa mkuu wa magereza mkoa wa
Mwanza.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Shibula Mhe Swila Dede
amemshukuru Mhe Mbunge na kumuomba kuendelea kutatua kero zinazowakabili
wananchi wake hasa zile za fidia ya kutwaliwa maeneo yao.
Mkutano huo pia ulihusisha viongozi wa chama tawala (CCM) wa
wilaya na kata, wataalamu wa Manispaa ya Ilemela,wakala wa barabara vijijini na
mjini TARURA, shirika la umeme TANESCO, shirika la Maji MWAUWASA ambapo kila
mwananchi amekuwa akipata nafasi ya kuuliza maswali kwa wataalamu hao, kuhoji,
kupongeza, kukosoa, na kushauri juu ya shughuli za kimaendeleo zinazotekelezwa.
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imtolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
No comments:
Post a Comment