Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amewaasa
wananchi wake kutumia vizuri fursa ya urasimishaji wa makazi kwa kuwa zoezi
hilo lina ukomo.
Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza na wananchi wa mtaa wa
Buyombe kata ya Kahama ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kusikiliza kero za
wananchi, ushauri, na pongezi kwa shughuli za kimaendeleo zinazotekelezwa na
Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ambapo amewataka
wananchi hao kumshukuru Mhe Rais kwa kuleta zoezi la urasimishaji wa makazi
kupitia wizara ya ardhi hivyo kuwataka kutumia vizuri fursa hiyo kwa kuchangia
gharama za urasimishaji na kupata hati miliki kwani zoezi hilo si endelevu
litakoma mara baada ya kuzinduliwa kwa mpango kabambe wa matumizi ya ardhi kwa
jiji la Mwanza na baada ya hapo wananchi wote watatakiwa kujenga kwa kufuata
mpango huo kabambe wa matumizi ya ardhi na si vinginevyo.
‘… Ndugu zangu kwanza tunapaswa kumshukuru Mhe Rais anaewajali
wananchi wanyonge, Kupitia Wizara ya Ardhi ameleta zoezi la urasimishaji makazi
lakini hatutaki kuitumia vizuri fursa hii, hatutaki kuchangia gharama za
urasimishaji, Ndugu zangu tukumbuke kuwa zoezi hili si endelevu lina ukomo,
Ukisha zinduliwa tu mpango kabambe wa matumizi ya ardhi (masterplan) hatutakuwa
tena na zoezi la urasimishaji wa makazi …’ Aliwaasa wananchi hao.
Kabla ya kuanza kwa ziara hiyo Dkt Angeline Mabula alipata
wasaa wa kukutana na uongozi wa chuo kikuu cha Mzumbe katika ofisi za
halmashauri ya manispaa ya Ilemela wakiongozwa na makamu mkuu wa chuo Profesa
Lugano Gusiluka ambapo Profesa Gusiluka amemshukuru mbunge huyo na manispaa kwa
ujumla wake kwa ushirikiano wanaoutoa kwa chuo chake kwanza kwa kutoa eneo la
ujenzi wa kampasi ya chuo hicho huko kata ya Sangabuye wilaya ya Ilemela, Na
kuongeza kuwa mpaka sasa zoezi la ulipaji fidia limekwisha kamilika na muda si
mrefu taratibu nyengine zitafuata kuhakikisha
Kampasi hiyo inakamilika ili kutoa huduma kwa wananchi wa kanda ya Ziwa.
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
19.12.2018
No comments:
Post a Comment