Wananchi wametakiwa kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanalipa
kodi ili Serikali iweze kuwahudumia.
Kauli hiyo imetolewa leo na mbunge wa jimbo la Ilemela ambae
pia ni naibu waziri wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi
mheshimiwa Daktari Angeline Mabula wakati akizungumza na wananchi wa mitaa ya
Gedeli na Nyakato sokoni iliyopo katika
kata ya Nyakato ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kusikiliza kero,
changamoto na ushauri kutoka kwa wananchi wa jimbo lake ambapo ametumia fursa
hiyo kuwasisitiza juu ya umuhimu wa kulipa kodi ili Serikali iweze kuwahudumia
kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ule wa ununuzi wa ndege
mpya, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja,
mradi wa bwawa la kuzalisha umeme maarufu kama Striggers Gauge
‘… Tunaowajibu kama wananchi na mheshimiwa Rais kila siku
anazungumza tuko watanzania zaidi ya milioni 54 walipa kodi ni milioni 2,
Kwahiyo tunatakiwa kuona aibu, Hivi ni nani anaehudumia huduma za jamii zote
ambazo ziko hapa kama sio sisi wenyewe tunaotakiwa kulipa kodi …’ Alisema
Aidha Daktari Mabula ameipongeza idara ya ardhi ya manispaa
ya Ilemela kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kushughulikia kero na migogoro
ya ardhi huku akiwahakikishia wananchi wake kuwa hakuna ucheleweshwaji wa hati
miliki kama utakuwa umekidhi vigezo na masharti yote muhimu yanayohitajika.
Kwa upande wake afisa ardhi wa manispaa ya Ilemela ndugu
Shukrani Kyando amewataka wananchi waliokwisha milikishwa viwanja kuhakikisha
wanavilinda na kusisitiza kuwa si jukumu la serikali kisheria kulinda kiwanja
cha mtu baada ya kumilikishwa.
Nae Diwani wa kata ya Nyakato mheshimiwa Alfred Wambura
amemshukuru mbunge huyo kwa kuipa nafasi ya kipekee kata yake kwa kukubali
kufanya mikutano miwili kwa siku moja katika mitaa miwili tofauti ya kata ya
Nyakato huku akiahidi kumuunga mkono kwa kumpa ushirikiano.
Ziara ya Mheshimiwa Daktari Angeline Mabula imehudhuriwa pia
na wataalam wa manispaa ya Ilemela, wataalamu wa wakala wa barabara za mijini
na vijijini (TARURA), Shirika la Umeme nchini (TANESCO), shirika la maji safi
na maji taka (MWAUWASA), viongozi wa dini na wa chama tawala chama cha
mapinduzi ngazi ya wilaya na kata.
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga '
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
20.12.2018
No comments:
Post a Comment