Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ameiagiza bodi na menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
kujirekebisha kwa kuondokana na matumizi mabaya ya fedha na kuwasilisha
upya ombi lake la kutaka kibali cha kukopa fedha kwa ajili ya kumalizia
miradi yake ya ujenzi iliyokwama kutokana na ukosefu wa fedha.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 13 Desemba, 2017 katika sherehe
ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi wa Iyumbu Mjini
Dodoma baada ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Neemia Mchechu kuomba
Serikali itoe kibali kwa NHC kukopa Shilingi Bilioni 232 kwa ajili ya
kumalizia miradi minne mikubwa ya ujenzi wa majengo iliyopo Jijini Dar
es Salaam.
Pamoja
na agizo hili Mhe. Rais Magufuli pia amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na Bodi ya NHC kuchukua hatua
dhidi ya migogoro iliyopo ndani ya shirika hilo ikiwa ni pamoja na
kuwaondoa watendaji wanaoleta chokochoko.
Hata
hivyo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Neemia
Mchechu na wafanyakazi wa NHC kwa kazi nzuri wanazofanya ikiwemo ujenzi
wa nyumba katika maeneo mbalimbali nchini na kuongeza ukusanyaji wa
mapato kutoka Bilioni 34 hadi 154.
“Mambo
mengi mnafanya vizuri, naifahamu NHC najua mmepiga hatua kubwa ya
kujenga nyumba sehemu mbalimbali, lakini jirekebisheni kwenye matumizi
ya fedha, nataka Waziri Lukuvi ukakae na bodi ya NHC na Mkurugenzi Mkuu
mfanye tathmini na mniletee maelezo ya namna mtakavyozirudisha hizo
Shilingi bilioni 232 mtakazokopa, nikipata maelezo vizuri nitatoa
maelekezo Wizara ya Fedha na Mipango iwape kibali” alisisitiza Mhe. Rais
Magufuli.
Mapema
akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Neemia Mchechu
amesema katika awamu ya kwanza mradi wa makazi wa Iyumbu unajenga nyumba
300, ambapo 150 zimekamilika na zimeshanunuliwa na nyingine 150 ujenzi
wake umeanza.
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amemshukuru
Mhe. Rais Magufuli kwa kuanzisha ujenzi wa nyumba za makazi Dodoma hata
kabla ya mradi wa Iyumbu na amebainisha kuwa ili kuwafikia Watanzania
wengi ameshatoa maelekezo kwa NHC kuachana na ujenzi wa majengo marefu
na badala yake kujielekeza katika ujenzi wa nyumba za kawaida
zitakazouzwa kwa gharama nafuu.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameufuta mpango wa kuwepo eneo la makaburi
ya viongozi na kuagiza eneo lenye ukubwa wa ekari 129 katika kata ya
Iyumbu lililochukuliwa na Serikali lirudishwe kwa wananchi na waruhusiwe
kulitumia kwa shughuli zao.
Mhe.
Rais Magufuli pia ametaka mchakato wa kubadili sheria ya makaburi ya
viongozi wa kitaifa ufanye kwa kuwa amejiridhisha kuwa viongozi wote
hawana nia ya kuzikwa katika eneo hilo.
Sherehe
za uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa makazi wa Iyumbu Mjini Dodoma
umehudhuriwa na Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Naibu Spika Dkt.
Tulia Ackson, Mawaziri na Naibu Mawaziri na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma

No comments:
Post a Comment