Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umefanya uhakiki wa kura zilizopigwa katika uchaguzi wa jumuiya hiyo ngazi ya Taifa na kubaini kuwa viongozi wote waliochaguliwa wamechaguliwa kihalali.
Aidha umetoa onyo kwa wale wote wanaojivika joho la kuwa wasemaji wa jumuiya kuacha mara moja kwa kuwa mamlaka za usemaji zipo kwa mujibu wa kanuni na katiba.
Kaimu katibu wa UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma amesema kama jumuiya walipokea agizo kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais John Pombe Magufuli kufanya uhakiki upya ili kujiridhisha iwapo haki imetendeka na kila mmoja amepata anachostahili zoezi ambalo limekamilika na tayari wameshakabidhi taarifa ya uhakiki huo katika mamlaka za chama.
Amesema zoezi hilo walilifanya kwa kushirikiana na vyombo vya dola ambavyo vina mamlaka ya kusimamia heshima na nidhamu na kusisitiza kuwa UVCCM imesimamia uchaguzi huo kwa haki na usawa na umakini mkubwa na kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele bila ya kufanya ubabaishaji na hila vile wana dhamira ya dhati kumuunga mkono Rais Magufuli.
" Tunaposema tunamuunga mkono Rais Magufuli sio kwa maneno ni kwa vitendo katika hili Rais Magufuli ni muumini wa kweli wa kusimamia haki na usawa hapendi wala hayuko tayari kuona mambo ya hovyo yakifanywa ili kumuumiza mwanachama au mtu yeyote tunamshukuru sana na kumpongeza Mwenyekiti Magufuli" alisema Shaka
Hata hivyo Shaka amekiri uwepo wa matatizo madogo sana wakati wa kuweka kura matatizo ambayo kwa namna moja ama nyingine hayakuwaondolea ushindi waliotangazwa ambao wameshinda kihalali kabisa
Amesisitiza na kukuendelea kuwaomba Vijana wote kuendelea na umoja, utulivu na mshikamano na kuungana pamoja na mwenyekiti mpya Kheir James katika kufikia dhamira ya dhati aliyonayo kufanyia mabadiliko makubwa umoja huo kimfumo, kiutawala na kiutendaji.
Katika uchaguzi wa UVCCM ngazi ya Taifa uliofanyika jumapili tarehe 10 Disemba mwaka huu ndugu Kheir James alichaguliwa kwa kura 319 kati ya kura 583 pamoja na wajumbe NEC wajumbe wa baraza na wajumbe wa kuwakilisha katika jumuiya za UWT na Wazazi.

No comments:
Post a Comment