Wataalamu wa ardhi na mipango miji wameaswa kutokaa ofisini na badala yake wawafuate wananchi kule walipo kwaajili ya kuwasikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero na changamoto za ardhi zinazowakabili wananchi hao.
Kauli hiyo imetolewa leo na mbunge wa jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Nyasaka wilaya ya Ilemela ambapo amewataka wataalamu wote wa ardhi kuhakikisha wanawafuata wananchi kule walipo kwaajili ya kutatua changamoto za ardhi ili kupunguza migogoro ya ardhi isiyokuwa na tija pamoja na kuwaomba wananchi kuhakikisha wanalipa kodi za ardhi ili Serikali ipate fedha za kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo
‘… Kwa upande huu wa ardhi nilishawahi kuelekeza wataalamu wa ardhi wapange siku za kwenda kwa wananchi kwenye kata zao kusikiliza kero na changamoto za ardhi ili wazipatie ufumbuzi walau hata mara mbili kwa wiki hii itapunguza migogoro isiyokuwa ya msingi …’ Alisema.
Aidha Mhe Dkt Mabula mbali na kusisitiza juu ya umuhimu wa zoezi la urasimishaji makazi, amekemea vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo huku akiongeza kuwa Serikali haitavumilia mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na unyama huo kwa watoto wadogo sambamba na kuwataka viongozi wa mitaa kutekeleza wajibu wao wa kuitisha vikao vya kisheria na taratibu vya kukutana na wananchi kusoma mapato na matumizi na kujadili utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu Amosy Zephania ametaja miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali kwa kushirikiana na mbunge wa jimbo hilo ndani ya kata ya Nyasaka ikiwemo ujenzi wa madarasa 9 huku mbunge wa jimbo hilo akitoa tofali za ujenzi huo, ujenzi wa barabara ya Nyamuge uliogharimu zaidi ya milioni 160 mpaka sasa, uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya kinamama, vijana na walemavu ambapo zaidi ya milioni 24 mpaka sasa imeshatolewa, sanjari na kutenga milioni 115 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwaajili ya kukarabati miundombinu ya madaraja na barabara za Nyasaka-Nyamuge (milioni46), Nyasaka-Nyamuge-Angelos (milioni 10.2), Nyasaka Islamic (milioni 21) daraja la Nyasaka Center (milioni 38) pamoja na uboreshaji wa soko jipya la kata hiyo.
Pia kupitia kikao hicho Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amemshukuru Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa fedha za ujenzi wa Kivuko cha MV Mwanza chenye uwezo wa kubeba watu 1000,mizigo tani 200, kilichogharimu shilingi bilioni 8.9 na fedha za ujenzi wa mradi mkubwa wa maji kwa wilaya za Ilemela na Nyamagana wenye jumla ya shilingi Euro milioni 30.
‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
30.07.2018
No comments:
Post a Comment