Timu ya Kata ya Nyamhongolo imeendelea kufanya vizuri katika mashindano ya mpira wa miguu ya Angeline Jimbo Cup 2018 yaliyoasisiwa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji vya vijana wa jimbo la Ilemela.
Katika mchezo wake wa leo Agosti 16, 2018 dhidi ya Timu ya Kata ya Kahama, Timu hiyo imefanikiwa kufunga magoli matatu goli la kwanza likifungwa dakika ya 27 na mchezaji aliyejulikana kwa jina la Mohamed Aziz 27 kabla ya mchezaji Bernard James kuiongezea goli la pili dakika ya 30 hatimae dakika ya 90 mchezaji Andrea Michael kuhitimisha kwa kufunga goli la tatu, wakati mahasimu wao Timu ya Kata ya Kahama wakiambulia magoli mawili yaliyofungwa na Regan Peter dakika ya 12 na baadae Faustine Peter kuiongezea goli la pili mnamo dakika ya 36.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Diwani wa Kata ya Nyamhongolo Mhe Andrea Nginila mbali na kumshukuru mbunge wa jimbo hilo kwa kuanzisha mashindano hayo ametamba kuchukua ubingwa, Pamoja na kuwaasa vijana wa kata yake kuitumia vizuri fursa ya uwepo wa mashindano hayo ili kujipatia ajira kwa kujiunga na Timu kubwa kwani michezo mbali na kuwa na umuhimu kwa afya lakini pia ni ajira kama kauli mbiu ya mashindano hayo inavyosema.
Timu ya Kata ya Kahama imezidi kufanya vibaya katika mashindano ya Angeline Jimbo Cup 2018 kwani hii ni mechi ya pili kufungwa mfululizo mara baada ya mechi iliyopita kuambulia kipigo cha magoli mawili kwa sifuri kutoka kwa Timu ya Kata ya Nyakato. Hata hivyo Mwalimu wa Timu hiyo anayejulikana kwa jina la Cosmas Mtobeka ameahidi kufanya vizuri katika mechi zinazofuata kwa kurekebisha makosa yote yaliyojitokeza katika michezo yake ya awali.
Wakati huo huo mechi iliyochezwa katika kiwanja cha Sabasaba kwa kuzikutanisha Timu ya Kata ya Nyasaka na Timu ya Kata ya Buzuruga imeisha kwa Timu ya Kata ya Buzuruga kuinyuka vikali Timu ya Kata ya Nyasaka magoli matatu kwa magoli mawili, Huku mechi iliyochezwa kiwanja cha Kona ya Bwiru ikiisha bila kuwepo mbabe kwa Timu ya Kata ya Kitangiri na Timu ya Kata ya Ibungilo kufungana goli moja kwa moja., Wakati kiwanja cha Shule ya msingi Bugogwa kilichoikutanisha Timu mwenyeji Kata ya Bugogwa na Shibula nazo zikitoka sare kwa kufungana goli moja kwa moja.
‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
No comments:
Post a Comment