Saturday, September 22, 2018

DKT ANGELINE MABULA AWASILI UKARA WILAYANI UKEREWE KUWAFARIJI WAHANGA AJALI YA MV NYERERE.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amefika kisiwa cha Ukara Wilayani Ukerewe kwa lengo la kutoa pole na kuwafariji wafiwa na majeruhi wa ajali ya Meli ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, 2018 wilayani humo.

Akizungumza mara baada ya kuwasili kisiwani humo, Mhe Dkt Angeline Mabula amempa salamu za pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe John Mongela, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe Boniphace Maghembe na Wananchi wote walioguswa na tatizo hilo kwa namna moja ama nyengine huku akiwataka kuwa wavumilivu na kuungana pamoja katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na ndugu zetu kwa kuwaombea waliofariki na wale majeruhi ili waweze kupona kwa haraka

' Binafsi nimeguswa sana na msiba huu mzito kwa taifa letu, Na kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Ilemela tunatoa pole kwa wananchi wenzetu walioguswa na kadhia hii kwa namna moja ama nyengine ...'

Aidha Mhe Dkt Angeline Mabula ameongeza kuwa sehemu kubwa ya jimbo la Ilemela ni maji hivyo kutoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo kutoa taarifa katika mamlaka husika pindi wanapoona ukiukwaji wa sheria na taratibu za usafiri wa majini sanjari na kueleza namna ajali hiyo ilivyogusa wananchi wake ambapo mpaka sasa watu wawili wakazi wa Ilemela wameripotiwa kufariki katika ajali hiyo akiwemo Mwalimu Albert Mongela na mkewe.

Pamoja nae Mhe Dkt Angeline Mabula alikuwepo   Mbunge wa Viti Mwalimu Mhe Kemmy Lwota, Waziri wa Kilimo Mhe Charles Tizeba, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe Kangi Lugola na Mkuu wa Majeshi Charles Mabeho.

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'

Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
22.09.2018.






No comments:

Post a Comment