Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) imewataka aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Klabu ya Simba, Zacharia Hans Pope na
Frankline Lauwo kujisalimisha katika ofisi zake au kituo cha polisi
kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kauli
hiyo imetolewa leo Ijumaa Septemba 14, 2018 na naibu mkurugenzi mkuu wa
Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo katika mkutano wake na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amedai kuwa Hanspope alitoa taarifa za uongo kuhusu malipo ya kodi.
Amesema
Zacharia kwa kushirikiana na washtakiwa wengine Evans Aveva, Geofrey
Nyange 'Kaburu' walitoa maelezo ya uongo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kwamba klabu ya Simba imenunua nyasi bandia kutoka Kampuni ya
Ninah Guangzhou Trading zenye thamani ya Dola 40,577 za Marekani,
maelezo ambayo yalikuwa ya uongo kwani nyasi hizo zilinunuliwa kwa dola
109,499.
Kuhusu
Lauwo, Mbungo amesema alifanya kazi ya ukandarasi wa ujenzi wa uwanja
wa mpira wa miguu wa Simba uliopo Bunju, Kinondoni jijini Dar es Salaam
kwa Sh249, 929,704 wakati akiwa hajasajiliwa katika Bodi ya Makandarasi
Tanzania.
"Tumewatafuta kwa njia za siri na uwazi bila mafanikio. Tunawataka kuripoti kituo cha Takukuru au polisi,"amesema Mbungo.
"Mwananchi atakayefanikisha kupatikana kwa watu hawa atapatiwa zawadi.”

No comments:
Post a Comment