Thursday, October 4, 2018

ILEMELA TUNA MBUNGE ANAETAMBUA WATUMISHI WAKE

Diwani wa Kata ya Kawekamo Mhe Japhes Rwehumbiza amempongeza na kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kutambua umuhimu wa watumishi wa idara ya elimu na kumpa ushirikiano katika kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Idara hiyo ndani ya kata yake ikiwemo mchakato unaoendelea wa kuhakikisha watumishi wa Idara hiyo wanapata viwanja vya makazi kwa gharama nafuu. 

Akizungumza katika kikao kazi kilichojumuisha walimu wa shule za msingi na sekondari za binafsi na Serikali zilizopo ndani ya kata hiyo, viongozi wa chama cha walimu wilaya ya Ilemela (C.W.T), wataalamu wa kata ya Ilemela, muwakilishi wa jeshi la polisi, afisa elimu michezo wa manispaa ya Ilemela ambae pia ndie mlezi wa kata hiyo, na wenyeviti wa bodi za shule, Mhe Japhes Rwehumbiza amezitaka bodi za shule kutekeleza wajibu wake katika kusimamia shule zao pamoja na kutambua mchango wa mbunge wa jimbo hilo wa kutoa vitabu vya masomo ya Sayansi kwa shule za kata yake, kutoa matofali ya ujenzi wa madarasa na ofisi za walimu  pamoja na kutoa viti na meza kwenye ofisi za walimu wa shule ya sekondari Kilimani

‘.. Niwahakikishie tunae mbunge anaetambua watumishi wake, nyie wenyewe ni mashahidi kwa namna mama huyu anavyopambana kwa kushirikiana na sisi wasaidizi wake katika kutatua changamoto za watumishi na wananchi wake ..’ Alisema 

Aidha Mhe Japhes Rwehumbiza ameahidi nyumba ya kuishi bure kwa kipindi cha miezi sita kwa mtumishi yeyote atakaepangiwa kufanya kazi katika kata yake, huku akiwapongeza walimu wote wa manispaa ya Ilemela kwa uadirifu na weredi waliouonesha katika kusimamia zoezi la mitihani ya darasa la Saba hivyo kuifanya wilaya ya Ilemela kutokuwemo katika kashfa ya uvujaji wa mitihani, Jambo linaloiletea sifa na heshima wilaya hiyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha walimu (C.W.T) wilaya ya Ilemela, Mwalimu Mateseko Benjamin Bulugu mbali kushukuru, amempongeza mbunge wa jimbo la Ilemela na diwani wa kata hiyo huku akiwataka walimu wenzake kuendelea kushirikiana na viongozi hao katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu katika maeneo yao sanjari na kuwaasa watumishi hao kuacha kulalamika pembeni badala yake watumie Ofisi za chama chao katika kupata haki.

Nae afisa elimu michezo wa wilaya ya Ilemela Mwalimu Kizito Bahati Sosho amewaasa walimu wa wilaya hiyo kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kisha kudai haki badala ya kulalamika bila ya kutimiza majukumu wanayostahili kuyatekeleza.








No comments:

Post a Comment