Mbunge wa jimbo la Ilemela Mheshimiwa Daktari Angeline
Mabula ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha afya Lumala kilichopo kata
ya Ilemela na kugharimu zaidi ya shilingi 40,490,000 kikiwa katika hatua ya
kukamilika kwa Boma.
Akizungumza na wananchi wa mtaa wa Lumala Daktari Mabula
amewapongeza wananchi hao kwa utayari wao wa kuunga mkono jitihada za Serikali
katika kusogeza huduma muhimu kwa jamii kwa kukubali kuchangia kiasi cha
shilingi 6,990,000 kilichotumika kwaajili ya kukamilisha msingi wa kituo hicho
kabla ya yeye kutoa matofali yote ya ujenzi wa boma la kituo hicho
‘… Niwapongeze sana wana Lumala ni mitaa michache sana
ambayo wananchi wake wako teyari kujitokeza na kuchangia ujenzi wa miundombinu
muhimu kama shule na zahanati, Wengi wanangojea Serikali ifanye na ndio maana
mliponifata kunishirikisha sikusita kwa sababu niliona nguvu yenu …’ Alisema
Aidha Mheshimiwa Mabula amemuomba mkurugenzi wa manispaa ya
Ilemela kuhakikisha anamalizia hatua iliyobaki ya kupaua jengo hilo kama wanavyoshirikiana katika kutekeleza
miradi mingine ya maendeleo, Kwa sera ya utatu kwa maana ya wananchi kuchangia
gharama za msingi, mbunge kujenga boma na manispaa kupaua.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ilemela Mheshimiwa Wilbard
Kilenzi amemshukuru mbunge huyo kwa kuunga mkono jitihada za wananchi wa kata
yake huku akimuomba kuendelea kutoa msukumo kwa ngazi husika ili kituo hicho kiweze kufunguliwa kwa
wakati uliokusudiwa.
Mara baada ya uwekaji jiwe la msingi mheshimiwa mbunge
ameendelea na ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi, changamoto, ushauri na
kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa ujenzi wa viwanja
vya michezo ya mpira wa miguu, mpira wa mikono, na mpira wa pete vinavyojengwa
eneo la Sabasaba katika kata hiyo akiambatana na viongozi wa shirika la maji
safi na mazingira MWAUWASA, shirika la umeme TANESCO, wakala wa barabara za
vijijini na mjini TARURA, wakuu wa idara za manispaa ya Ilemela, viongozi wa
vyama vya kisiasa na dini.
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
24.12.2018









No comments:
Post a Comment