Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeitikia wito wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula katika kuhakikisha anamaliza kabisa tatizo la uhaba wa Vyumba vya Madarasa kwa kutoa pesa taslimu shilingi Milioni Mia Moja Sabini na Tano (175,000,000/=) kwa ajili ya Ujenzi wa Vyumba vya madarasa kwa Shule 7 za msingi ambazo ni Shule ya msingi Bulola, Buhila, Igombe, Kisundi, Kahama, Kitangiri, na Nyamhongoro ambapo kila shule imepokea kiasi cha shilingi Milioni Ishirini na Tano (25,000,000=).
Aidha kufuatia hatua hiyo Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula
amemshukuru Mhe Rais Dkt John Magufuli kupitia Wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Mhe Suleiman Jaffo kwa kuitikia ombi lake na kulifanyia kazi kwa uharaka huku akiwataka viongozi wengine wa kata na Mitaa kuendelea kuhamasisha wananchi kuchangia nguvu zao ili fursa iliyopatikana iwe na tija katika kuondoa adha ya watoto kusongamana katika vyumba vichache vilivyopo sasa.
'.. Mradi wa tofali umekuwa kichocheo kikubwa na ufumbuzi wa changamoto ya miundombinu jimboni, Hivyo nawaomba wananchi waendelee kuchangia maendeleo yao kwa kuenzi kauli mbiu yetu ya Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga ..'
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela.



No comments:
Post a Comment