Serikali
imelipongeza Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa
ushirikiano wake na Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo hasa
katika sekta za Kilimo Afya na Maendeleo ya Jamii kwa kutumia wataalam
na uzoefu kutoka Japan.
Pongezi
hizo zimetolewa Jijini Dar es Salaam leo na Mkurugenzi Msaidizi wa
ushirikiano wa kiufundi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Bw.Msafiri Marwa alipokuwa akiwaaga vijana wa
kijapani waliokuwa wanajitolea katika sekta ya Kilimo na Maendeleo ya
jamii hapa nchini.
“Serikali
ya Japan kupitia shirika lake la JICA imekuwa na ushirikiano wa muda
mrefu na serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile
kuwajengea uwezo Watanzania kupitia ufadhili wa masomo ya elimu ya juu
nchini Japan na kuleta watu wa kujitolea katika miradi ya maendeleo hapa
nchini,” alieleza Bw. Marwa.
Aidha,
Bw.Marwa ambaye alimuwakilisha Naibu Katibu Mkuu Utumishi Bi. Suzani
Mlawi aliipongeza Japan kwa kutumia rasilimali watu pamoja na rasilimali
fedha kupitia JICA kufadhili utoaji wa huduma za kijamii jambo ambalo
ni kipimo cha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Amewapongeza
vijana wa kijapan kwa kazi nzuri waliyoifanya hapa nchini katika
kipindi chote cha miaka miwili ya kuwahudumia watanzania hasa katika
sekta ya Kilimo na Afya.
“Kwa
niaba ya serikali niwapongeze vijana wote mliokuja hapa nchini kwa
kufanya kazi na jamii ya Watanzania, mmefanya kazi kwa jitihada kubwa
wakati mwingine katika mazingira magumu, niwahakikishie kuwa serikali ya
Tanzania itaendelea kuimarisha mazingira ya ushirikiano ili kuendeleza
uhusiano ” alifafanua Marwa.
Mkurugenzi
huyo pia aliwakumbusha vijana hao kuwa mabalozi wazuri nchini Japani na
mataifa mengine watakayokwenda ili kuwavutiwa wawekezaji na watalii
kuja kuwekeza katika shughuli za maendeleo pamoja na kuleta watalii
wengi kwani Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, mazingira rafiki kwa
wageni na amani ya kutosha.
Kwa
upande wake, Mratibu wa kundi la vijana wa kujitolea kutoka JICA
Bw.Ichiro Owa alisema kuwa, anaipongeza serikali ya Tanzania kwa
kuwapokea na kuwapa ushirikiano na ulinzi wa kutosha vijana waliokuja
kujitolea katika shughuli za maendeleo kwa siku zote ambazo wamekuwa
hapa nchini.
“Mpango
wetu kwa sasa ni kuleta vijana wengi zaidi wa kujitolea kwasababu ya
ushirikiano tulioupata kutoka kwa serikali ya Tanzania ni mzuri kwani
tumefurahia usalama amani na utulivu pamoja na ukarimu wa watanzania ”
alifafanua Bw. Owa.
Mratibu
huyo wa vijana wa kujitolea kutoka Japan alisema ushirikiano kati ya
nchi yake na Tanzania ni wa kihistoria na umekuwa wa manufaa kwa pande
zote mbili, aliongeza kuwa kwa mwaka huu, JICA ina jumla ya vijana 40
wanaojitolea na matarajio yao ni kuongeza vijana kati ya 60 hadi 70 kwa
mwaka ujao.
Vijana
wa kujitolea walioagwa katika hafla hiyo ni pamoja na Kyoko Tada
aliyekuwa akifanya kazi ya Uuguzi katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, Shu Sato aliyekuwa katika Ofisi ya Kilimo Wilaya ya Siha
Mkoani Kilimanjaro na Yusuke Sakakibara aliyekuwa anafanya kazi ya
maendeleo ya jamii katika Wilaya ya Masasi.
JICA
ilianza mpango wake wa kuleta vijana wa kujitolea katika shughuli
mbalimbali za maendeleo mwaka 1967 ambapo takwimu zinaonyesha kuwa tangu
kuja kwa kundi la kwanza kutoka Japani idadi imeongezeka kufikia vijana
1,568.
No comments:
Post a Comment