Sunday, October 29, 2017

WANANCHI WATAKIWA KUCHANGIA DAMU KUOKOA MAISHA JIJINI MWANZA

Wananchi wa  Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza wametakiwa kujitoa kwa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wengine sambamba na kujiwekea akiba pindi unapotokea uhitaji kwao binafsi.

Hayo yamesemwa leo na Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa Uzinduzi wa mradi wa Uthamini wa bidhaa za nyumbani uliyopewa jina la HOME KWANZA uliohusisha makundi ya Vijana wazalishaji wa bidhaa mbalimbali na wasanii wa maigizo, muziki, uchoraji kwa kuonyesha shughuli zao na kisha kuchangia Damu katika kuokoa maisha na kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli.

Na mimi najua kuwa ukichangia damu maanake umeokoa maisha, lakini pia ukichangia damu wewe mwenyewe unakuwa umejiandalia kesho yako huwezi kujua lini utapata tatizo la kuhitaji damu, huwezi kujua lini utapata ajali, huwezi kujua lini ndugu yako wa karibu atapata shida, Kwa hiyo unachotakiwa kujua ni kwamba unachangia kwaajili ya akiba na pia unaokoa maisha …’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Angeline Mabula ameongoza Vijana waliojitokeza katika Uzinduzi huo kwa yeye kuchangia Damu sambamba na kufafanua juu ya umuhimu wa kuchangia Damu mbali na kuokoa maisha   akitaja kujua afya zao na kujiepusha na magonjwa yanayotokana na kuzidi kwa Damu mwilini.

Kwa upande wake muwakilishi kutoka Damu Salama ndugu Emanuel Ndaki amewahakikishia wananchi waliojitokeza katika kuchangia Damu kuwa zoezi hilo linaendeshwa kitaalamu hivyo hawapaswi kuwa na hofu yeyote na taarifa zote zinabaki kuwa siri.

Akihitimisha  muasisi wa Mradi wa Home Kwanza na mmiliki wa White Fish Entertainment  Ndugu Frank Nubi mbali na kumshukuru Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kuwaunga mkono na ushiriki wake wa tangu kuasisiwa kwa mradi huo amemuomba Mbunge huyo kuendelea kuwaunga mkono Vijana katika kutumia Vipaji vyao kwa kuleta maendeleo na kujikwamua kiuchumi sambamba na kuthamini bidhaa zinazozalishwa nyumbani.

‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
29.10.2017



No comments:

Post a Comment