Mwandishi Yusuph Ludimo
Wananchi wanaoishi wilaya ya Ilemela wametakiwa kuunga mkono jitihada za utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazofanywa ndani ya wilaya yao kwa kushauri na kusaidia ufanikishaji wa miradi mbalimbali .
Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela John Wanga akiwa kata ya Bugogwa ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kwa kata za manispaa ya Ilemela anayoifanya kila baada ya miezi mitatu kwa kuambatana na wataalamu wa manispaa yake na viongozi mbalimbali kwenda kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi wa papo kwa hapo baadhi ya changamoto na kero zinazowakabili wananchi
‘… Ndugu zangu wananchi sisi tusiseme sana juu
ya mafanikio ya miradi tunayoitekeleza lakini pia tunategemea mengi tusikilize
kutoka kwenu, mtuambie, tushauriane, Tusiishie kulalamika tu kwasababu mnaweza
mkatushauri pia kwamba sisi tunafikiri tukifanya hivi tunaweza tukaboresha
zaidi …’ Alisema
Aidha Mkurugenzi Wanga ametaja miradi mbalimbali
inayoendelea kutekelezwa kwa kata ya Bugogwa ikiwemo zoezi la urasimishaji
makazi, ujenzi wa majengo ya zahanati ya Karume katika kuhakikisha huduma za
afya na huduma za mama na mtoto zinaimarika pamoja na mradi mkubwa wa
usambazaji maji unaoendelea na kuwafafanulia juu ya hatma ya mradi wa umeme wa
vijijini REA unaoendelea kutekelezwa katika vijiji vya kata hiyo huku akiwataka
kumuunga mkono Mhe Rais Dkt John Magufuli, mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula na madiwani kwa namna
wananvyosimamia na kusaidia ufanikishaji wa miradi hiyo na kuahidi mifuko ya
Saruji na Nondo za ujenzi wa daraja kwa wananchi wa mtaa Igombe B kama
watachangia mawe ya ujenzi huo
Kwa upande wake diwani wa kata ya Bugogwa Mhe William
Mashamaba mbali na kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa utekelezaji wa
miradi hiyo ya maendeleo katika kata yake amewahakikishia ushirikiano katika
kuhakikisha inafanikiwa tena kwa wakati huku akiwataka wananchi wake kufuata
sheria na taratibu ili kujiepusha na usumbufu usiokuwa wa lazima
Akihitimisha mkutano wa ziara hiyo mstahiki meya
wa manispaa ya Ilemela na diwani wa kata jirani na Bugogwa ya Sangabuye Mhe
Renatus Mulunga amewakumbusha wananchi hao juu ya umuhimu wa kuchangia shughuli
za maendeleo ikiwemo utaratibu wa manispaa yake wa kusaidia kumalizia miradi
inayoanzishwa na wananchi wenyewe huku akitolea mfano wa kuezekwa kwa msaada wa
manispaa kwa jengo litakalokuwa limefikia hatua ya boma litakalojengwa kwa
nguvu za wananchi
‘ Ilemela ni yetu,
tushirikiane kuijenga’








No comments:
Post a Comment