Mwandishi Yusuph Ludimo
Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amewataka
wananchi kuwa wazalendo kwa kuwafichua wasio raia wa Tanzania katika
zoezi la uandikishaji vitambulisho vya Taifa
Mhe Dkt Angeline Mabula ameyasema hayo alipofanya ziara ya
kushtukiza katika kituo cha uandikishaji wa vitambulisho vya taifa
(NIDA) kilichopo ofisi ya kata ya Ibungilo ambapo amewaasa wananchi
waliokuwa wamepanga foleni kwaajili ya zoezi hilo kuwa makini na
waangalifu katika ujazaji wa fomu za maombi sanjari na kuwaripoti wale
wote wasiostahili wakitaka kutumia mwanya huo kujipatia vitambulisho
hivyo huku akiwaelimisha juu ya umuhimu wa kuwa na kitambulisho hicho.
‘… Lazima muwe makini mnapojaza taarifa zenu lakini lingine
sisi ni wa Tanzania tunatakiwa kuwa wazalendo kama unajirani yako
ambaye si Mtanzania na amepanga foleni kutaka kupata kitambulisho cha
taifa toa taarifa mapema, Tusiwape watu wasiohusika ni nyinyi
wakuisaidia Serikali vinginevyo vitambulisho vyetu vitachukuliwa na watu
wasiokuwa waTanzania …’ Alisema.
Kwa upande wake msimamizi wa mamlaka ya vitambulisho vya
taifa (NIDA) kata ya Ibungilo Ndugu Eric Elisha mbali na kueleza juu
ya mwenendo wa zoezi hilo kwa kata anayoisimamia amemuhakikishia mbunge
huyo umakini na uzingatiaji wa haki kuhakikisha kila mwananchi
anayestahili anapata kitambulisho.
Nao wananchi waliojitokeza katika zoezi la uandikishaji
wamemshukuru Mhe Mbunge kwa kufanya ziara hiyo ya kushtukiza kukagua
mwenendo wa zoezi huku wakiwasilisha changamoto wanazokutana nazo na
kumuomba kuwasaidia namna ya kuzipatia ufumbuzi
Ziara hiyo ya gafla pia ilihusisha kulitembelea na
kuzungumza na wafanya biashara wa soko kuu la wilaya hiyo la Kiloleli
kujua changamoto wanazokutana nazo ili kuzipatia ufumbuzi huku akiwaasa
wale wote wanaofanya biashara nje ya soko kurudi sokoni hapo kwani
nafasi bado zipo zakutosha.
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa naOfisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
14.01.2018







No comments:
Post a Comment