Mwandishi Yusuph Ludimo
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wametakiwa kutowafumbia
macho Viongozi wanaoshirikiana na Wataalamu katika kuhujumu miradi ya
maendeleo inayotekelezwa na Serikali yao.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt
Angeline Mabula wakati akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM
kwa kata ya Nyamhongolo na Nyakato kueleza utekelezaji wa Ilani ya
uchaguzi ambapo amefafanua juu ya mambo aliyoyafanya kwa kipindi cha
miaka miwili katika eneo lao ikiwa ni ujenzi wa Matundu 12 ya Vyoo,
Ujenzi wa madarasa 3 na Madawati 160 kwa shule ya msingi Ibeshi,
Ugawaji wa Mifuko 70 ya Saruji na tofali 4750 za ujenzi wa Zahanati ya
Nyamadoke, Ujenzi wa gati 7 za Maji, Ujenzi na ufunguzi wa kisima cha
maji kinachotumia nishati ya Jua Nyamadoke, Ugawaji wa Vitabu vya
Sayansi na utoaji wa elimu ya Ujasiriamali kwa vikundi 34 huku akiwataka
kuwaumbua na kuwachukulia hatua wale wote wanaohujumu na kukwamisha
miradi ya maendeleo.
‘… Mnatakiwa kuwa macho kwenye miradi inayotumia fedha za
Umma na msione aibu kusema kwa maana ya nyinyi ambao mmetupa dhamana
sisi ya kuitekeleza Ilani, Kuna wengine wahandisi humu hata kama
hamfanyi kazi si mnaona miradi ya chini ya kiwango sasa lazima kutoa
taarifa kwa kumwambia mhusiaka palepale…’ Alisema.
Aidha Mhe Mbunge ameshukuru na ametaja mafanikio na miradi
mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe Rais
Dkt John Magufuli ikiwemo ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa viwanda,
ujenzi wa reli ya kisasa, utoaji elimu bure, urasimishaji makazi na
upangaji miji kupitia wizara ya Ardhi zoezi litakalofika ukomo mwezi
Juni 30 mwaka huu, upanuzi wa uwanja wa ndege, ongezeko la ukusanyaji
wa mapato, ongezeko la bajeti ya afya vitu ambavyo vitamsaidia Mtanzania
kutoka kwenye umasikini sambamba na kuufanya mkoa wa Mwanza kuwa
kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika ya Mashariki hivyo kuwataka
wananchi wake kuitumia vizuri fursa hiyo.
Kwa upande wake Muwakilishi wa Uongozi wa CCM wilaya ya
Ilemela aliyeambatana na Mbunge huyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
wilaya Ndugu Denis Lekela Kankono mbali na kupongeza jitihada za
utekelezaji wa Ilani ametaka kuchukuliwa hatua kwa watendaji wote wa
Serikali wasiokuwa waadirifu huku akiomba wanachama kuendelea kuunga
mkono na kutangaza mema yanayofanywa na Serikali yao.
‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa naOfisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
13.01.2018










No comments:
Post a Comment