Mwandishi Yusuph Ludimo
Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amefunga
mashindano ya ligi ya mpira wa miguu iliyohusisha Timu Saba kutoka Mitaa
ya Kata ya Kirumba iliyojulikana kama KIRUMBA SUPER CUP 2017 na
kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana
Taifa Comred Kheri James, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha
Mapinduzi wilaya ya Ilemela, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya
Kirumba na Diwani wa Kata hiyo Mhe Alex Ngusa
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia fainali ya
mashindani hayo iliyochezwa katika Uwanja wa Magomeni kata ya Kirumba
ikihusisha Timu ya MKOKOTENI FC na JURA FC Mhe Dkt Angeline Mabula mbali
na kuelezea historia ya Kata ya Kirumba katika kuzalisha wachezaji
nguli na tegemezi kwa vilabu mbalimbali vya soka nchini amewahakikishia
kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha anakuza vipaji vya vijana
ndani ya jimbo lake kupitia mashindano ya JIMBO CUP yanayofanyika kila
mwaka huku akisisitiza faida za michezo kwa jamii.
‘… Kwa hiyo unapocheza hapa huchezi kujifurahisha ni lazima
mtambue kuwa michezo ni afya michezo ni ajira, mbali na timu kubwa
zinazopita kuwatazama ili kuibua vipaji vipya nyie wenyewe mtakuwa
mmejikinga na maradhi mbalimbali …’ Alisema.
Aidha Mhe Dkt Angeline Mabula ameongeza kuwa mshindi wa
mashindano hayo atapata fursa ya kushiriki mashindano ya JIMBO CUP
mwaka huu wa 2018 yanayotarajiwa kuanza muda si mrefu sana kutoka sasa
Kwa upande wake muendeshaji wa mashindano hayo Ndugu
Mohamedi Rajabu amesema kuwa lengo la kuandaa mashindano hayo ni
kuwakutanisha watu karibu na kuibua vipaji vipya huku ikiwasaidia vijana
kutojiingiza katika mambo yasiyofaa ikiwemo uvutaji bangi na matumizi
ya madawa ya kulevya.
Fainali hiyo iliisha kwa Timu ya MKOKOTENI FC kuichapa Timu
ya JURA FC goli moja kwa sifuri, Goli lililofungwa dakika ya 38 kipindi
cha kwanza na mchezaji machachari Liberatus Mgeta na kuifanya timu yake
kuibuka kidedea na kujinyakuria Ng’ombe mnyama mmoja, Kombe na Jezi
seti moja zawadi iliyokabidhiwa na mgeni rasmi Dkt Angeline Mabula huku
Mwenyekiti wa Vijana UVCCM Taifa Kheri James akikabidhi Mbuzi mnyama na
mpira kwa mshindi wa pili Timu ya JURA FC.
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane ’
Imetolewa naOfisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
04.01.2018.







No comments:
Post a Comment