JESHI la Polisi mkoani Geita linawashikilia watu wawili wakazi wa
Kijiji cha Kasubuya wilayani Nyang’wale kwa kula njama wakiwa wazazi
kupokea mahari ya ng’ombe saba na kumwozesha mwanafunzi wa kidato cha
pili.
Binti huyo aliyekuwa anasoma katika shule ya sekondari Nyijundu, sasa ana ujauzito.
Aliyethibitisha kukamatwa kwa wazazi hao wa pande zote mbili ni Kamanda
wa Polisi mkoa wa Geita, Mponjoli Lotson na kuwataja ni baba mzazi wa
msichana huyo, Herman Makanika (48) na Maximillian Makila ambaye ni baba
mzazi wa mtuhumiwa aliyemuoa mwanafunzi huyo.
Ingawa hakulitaja jina la mtuhumiwa, Kamanda Mpojoli alimpongeza mwalimu
wa shule ya sekondari aliyetoa taarifa za kuwapo kwa tukio hilo na
akabainisha jinsi wazazi wa pande zote mbili walivyoshiriki kutenda
kosa licha ya mtuhumiwa kutoroka.
Alisema wazazi wa pande zote mbili wanahusika ingawa mtuhumiwa (muoaji)
anaendelea kusakwa, hivyo wanapaswa kuwajibika kutokana na kufanya
makubaliano kwa kutoa mahari ya ng’ombe saba na mzazi wa msichana
kuwapokea ng’ombe hao kama mahari.
Aliongeza kuwa baada ya polisi kuarifiwa ilichukua hatua za haraka na
watuhumiwa kukamawta na hadi jana walikuwa wanaendelea kushikiliwa huku
juhudi za kumsaka mtuhumiwa zikiendelea kuhakikisha anapatikana na
kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.

No comments:
Post a Comment