KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa
amefunguka kuwa amepata tetesi kuwa kuna mabaunsa wanaodaiwa wameletwa
jijini Dar kwa nia ya kuvuruga uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni
utakaofanyika kesho, Feb 17, 2018.
Mambosasa ameyabainisha hayo leo wakati akizungumza na wanahabari huku
akiwatoa hofu wananchi kuwa jeshi lake limejiandaa vizuri kwa ajili ya
kuimarisha ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi huo na kuwaonya
waliopanga kufanya vurugu kuwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
“Nimeambiwa kuna mabaunsa wameletwa kwenye uchaguzi huu, mimi sijawahi
kuona baunsa anayeweza kushindana na Serikali. Aliyejiandaa kupambana na
Dola namuonea huruma sana, hatabaki salama.
“Niwaambie tu kwamba, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
limejipanga vizuri kuimarisha ulinzi na usalama. Tutahakikisha usalama
unakuwepo, hakuna atakayefanya vurugu wakati wa uchaguzi,” Kamanda
Mambosasa alisema.

No comments:
Post a Comment