Ikiwa ni wiki moja imepita tangu Kiongozi wa Umoja wa Vyama vya Upinzani
nchini Kenya kujiapisha kuwa Rais wa watu wa nchini hiyo, Hatimaye Rais
wa Kenya anayetambulika kikatiba Uhuru Kenyatta amezungumza kwa mara ya
kwanza kuhusu tukio hilo.
Rais Kenyatta amesema kuwa kujenga taifa ni kazi kubwa lakini kubomoa ni
muda mfupi hivyo amemshauri Raila Odinga kuacha maneno yenye mizozo na
kuchafuana nje ya nchi kwani kushindwa kwenye uchaguzi ni jambo la
kawaida hata yeye alishawahi kushindwa na akajipanga tena.
“Kujenga ni ngumu lakini kupasua ni dakika moja, lakini hawaoni tabu
kupasua afadhali apasue apate uongozi, awe mkubwa, ukubwa sio kiti
ukubwa ukubwa ni vitendo ambavyo unawatendea wananchi ambao unataka
kuwaongoza, na hivyo hivyo hata sisi tumekuwa twahimiza ni nini
unawatendea wananchi wako. ukiwa umetoka nchi yako unaenda kutembea nchi
nyingine kusema wale wanaoongoza kule wanastahili kufungwa. Si uje hapa
Kenya kwetu utuambie,“amesema Uhuru Kenyatta huku akimshauri jambo la
kufanya Raila Odinga.
“Huwezi kufanikiwa kwa kumtakia mwenzio mabaya, omba mwenyezi Mungu na
uombe wananchi kwa njia tulivu uoneshe sera zako tofauti na sera za wale
wengine na wananchi sio wajinga wapo na ujuzi wakuamua ni nani wanataka
na nani hawataki. Kama hawakutaki safari hii we pumzika wacha wale
wengine waendelee, mimi nimegombea mara nyingi, mimi nimewahi kusimama
hii kiti nikashindwa na nikakaa nikatulia, Nikasema eehh Mwenyezi Mungu
basi hii sio nafasi yangu wakati hii na nikakubali kushindwa, sasa
ninaongoza na nitaongoza mpaka wananchi waseme basi wewe tulia, sasa
shida iko wapi na tunabaki tunachafuana hapa kila siku, Lets us work
together, Lets us keep Kenya moving ahead, lets us provide services to
our people mambo hayo ndiyo ya muhimu na ndivyo tutaendelea na waseme na
waseme hawatutishi,“amesema Rais Kenyatta kwenye kongamano la
kuimarisha hali ya usalama nchini Kenya liliofanyika wikiendi iliyopita
katika chuo cha Kenya School of Government (KSG) jijini Nairobi.

No comments:
Post a Comment