Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imewapiga marufuku wananchi wa
Tanzania kujichukulia sheria za barabarani mkononi kwa kuweka matuta
katika barabara bila ya kuvishirikisha vyombo husika kwa madai kitendo
hicho kinasababisha ajali.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Atashata Nditie katika
mkutano wa 10 kikao cha tano cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma
wakati alipokuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge Joseph
Kizito Mhagama alilotaka kufahamu serikali ina mpango gani wa
kumuwajibisha Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pale ambapo sababu
ya ajali inaonekana ni kutotekeleza utaratibu wa wakala huyo.
"Ni kweli kuna ubovu wa barabara na serikali imekuwa ikiendelea kufanya
jitihada za kurekebisha ubovu huo na kuhakikisha kwamba barabara zetu
kuu na zile za mikoa zinapitika kila wakati", amesema Nditie.
Aidha, Naibu Waziri huyo amedai kumekuwa na tabia ya hivi karibunui kwa
baadhi ya wananchi kujichukulia maamuzi mkononi kuweka matuta bila ya
kuambiwa.
"Kitendo hicho kimekuwa chanzo kimoja wapo cha ajali mbalimbali kwa
sababu wanapoweka matuta bila ya kuwashauri au bila ya kuwaambia
(TANROADS) inamaana yale matuta yanakuwa hayana alama na magari
yanapokuja yanafika na kuparamia yale matuta na kusababisha
ajali",amesisitiza Nditie.
Pamoja na hayo, Nditie ameendelea kwa kusema "niwashauri watanzania
wasiweke matuta barabarani bila ya kutoa taarifa kwa vyombo vinavyo
husika na barabara ili iwekwe alama ya kuwaoensha madereva kwamba kuna
tuta mbele wanapokwenda. Lakini nimwambie tu Mbunge Mhagama kwamba
Tanroads wanajitahidi sana kufanya kazi zao kwa uaminifu na umakini wa
hali ya juu wakizangatia usalama wa watanzania".
Kwa upand mwingine, leo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dkt.
Adelardus Kilangi ameapishwa rasmi kiapo cha uaminifu Bungeni ili aweze
kuitumikia serikali pamoja na wananchi wake kiujumla.

No comments:
Post a Comment