Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amemtaka kaimu Katibu Tawala
wa Mkoa wa Manyara, Arnord Msuya kumsimamisha kazi Ofisa Tarafa ya
Dongobesh, Bayo Banka kwa madai ya kushindwa
kutekeleza wajibu wake kutokana na kuchanganya siasa na kazi.
Pia, amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ambao
hawaungi mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuacha kazi
vinginevyo atawachukulia hatua kwa kutotimiza wajibu wao ipasavyo na
kuingiza siasa kazini.
Mnyeti ametoa agizo hilo jana Februari 5,2018 wakati akizungumza na
watumishi wa halmashauri hiyo katika ziara yake ya siku saba.
Amesema Banka anapaswa kusimamishwa kazi hadi hapo atakapotoa maelezo ya
kushindwa kutimiza wajibu wake kwa kuchanganya siasa na kazi.
Amebainisha kuwa CCM ilifanyika kampeni na kuinadi Ilani yake ya
uchaguzi kwa wananchi, kwamba kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa
Ilani hiyo kwa watumishi kuwatumikia wananchi.
"Mnakaa ofisini na kulipwa mishahara na posho nyingi lakini mnashindwa
kuwatumikia wananchi badala yake mnaingiza siasa chafu. Natoa onyo kwa
wote msirudie jambo hilo hata mara moja nitawachukulia hatua
kali,"amesema Mnyeti.
Mnyeti amesema anayo majina na taarifa za baadhi ya watumishi wanaofanya kazi kizembe na kuzorotesha shughuli za Serikali.
"Pamoja na ofisa tarafa huyo, pia nakukabidhi majina mengine ya
watumishi ambao wanatekeleza maagizo ya viongozi wa vyama vingine vya
kisasa badala ya kutekeleza maagizo ya viongozi wa Serikali inayoongozwa
na CCM," amesema Mnyeti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga
amesema watumishi wa halmashauri hiyo wamejipanga kuhakikisha
wanawatumikia wananchi ipasavyo.

No comments:
Post a Comment