Thursday, April 26, 2018

Benki ya AFDB kuwekeza zaidi Tanzania


Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dk Akinumwi Adesina ni miongoni mwa wageni wa kimataifa walioalikwa kuhudhuria maadhimisho ya miaka 54 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 2018.

Mbali na sherehe hizo, rais huyo aliyewasili nchini Aprili 25, 2018 atakuwa nchini kwa ziara ya siku tatu.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) alipokewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Dk Adesina ameahidi ndani ya miaka miwili ijayo, AfDB itawekeza Tanzania zaidi ya Dola 1.5 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh3.36 trilioni).

"Tuna uhusiano wa muda mrefu na Tanzania ambayo ni mnufaika anayeongoza kupata ruzuku na mikopo yenye masharti nafuu Afrika. Tangu mwaka 1971, AfDB imewekeza zaidi ya Dola 3.6 bilioni," amesema Dk Adesina katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha kwa vyombo vya habari.

Benki hiyo imefadhili mradi wa kusafirisha umeme wenye msogo wa kilovolti 400 wenye urefu wa kilomita 670 unaohusisha vituo vya kupozea umeme katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga kwa Dola 220 milioni.

AfDB pia inasaidia kutekeleza Mpango wa Kukuza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Sagcot).

Waziri Mpango amesema AfDB ni mshirika mkubwa wa maendeleo na licha ya kufadhili ujenzi wa barabara na nishati mwaka jana pekee ilitoa mkopo nafuu wa Dola 50 milioni kukuza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Dk Adeseina atatembelea mradi wa kupooza umeme uliopo Zuzu mkoani Dodoma.


No comments:

Post a Comment