Saturday, April 21, 2018

Magufuli kuzindua tawi la NMB, jengo la PSPF....Tazama Hapa Ratiba Nzima Ya Rais Magufuli

Rais John Magufuli kesho kutwa (Jumatatu) atazindua jengo la Mfuko wa Pensheni wa PSPF na tawi jipya la Benki ya NMB lililopo Mtaa wa Barabara ya Chimwaga mjini Dodoma.

Akizungumza leo  na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amesema Rais Magufuli atawasili kesho mjini hapa.

“Siku ya Jumanne Aprili 24, Rais atakuwa mgeni rasmi kulihutubia Bunge la Afrika Mashariki ambalo linafanyika Tanzania Bara hapa Dodoma,”amesema.

Amesema Alhamisi Rais atakuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitakazofanyika katika uwanja wa Jamhuri.

“Siku ya Ijumaa Rais atazindua barabara ya Dodoma hadi Babati yenye urefu wa Kilometa 231.8 na sherehe ya uzinduzi wa barabara hii zitafanyika kwenye wilaya ya Kondoa eneo la Bicha,”amesema.

Amesema uzinduzi wa barabara hiyo ni kichocheo kikubwa cha shughuli za uzalishaji na uchumi wa ukanda wote wa Bahi, Chamwino, Chemba na Kondoa.

“Nisisitize kuwa barabara hii ni sehemu ya Barabara kuu ya kaskazini (Great North Road) inayoanzia Cape Town Afrika Kusini hadi Cairo Misri hivyo ina umuhimu wa kipekee kwetu wananchi wa Dodoma upande wa shughuli za uzalishaji viwanda na uchumi,”amesema.

Dk Mahenge amesema Jumapili Rais ataondoka kulekea mkoani Iringa kwa ajili ya Sherehe za Mei Mosi kitaifa mwaka huu ambazo zinafanyika kitaifa mkoani humo.

“Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma namshukuru Rais Magufuli kwa heshima hii ya kipekee anayoendelea kutupatia sisi Mkoa wa Dodoma ambayo ni Makao makuu ya nchi,”amesema.


Amewataka wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kuhudhuria kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano na uzinduzi mwingine.

No comments:

Post a Comment