Serikali
imeonyesha dhamira yake ya dhati ya kutekeleza mkakati wa kuongeza
uwezo wa kuzalisha umeme baada ya kutenga Sh700 bilioni kwa ajili ya
mradi wa Stiegler’s Gorge, kwa mujibu wa bajeti ya Wizara ya Nishati
iliyowasilishwa bungeni jana.
Mradi
huo, uliopewa jina la mgunduzi wa Uswisi aliyefia eneo hilo mwaka 1907
baada ya kushambuliwa na tembo, utajengwa katika Mto Rufiji, ndani ya
Hifadhi ya Selous na unatarajiwa kuzalisha Megawati 2,100 za umeme.
Akiwasilisha
bajeti hiyo jana, Waziri wa Nishati, Dk Medrad Kalemani aliomba chombo
hicho cha kutunga sheria kiidhinishe Sh1.69 trilioni kwa mwaka 2018/19,
huku zaidi ya asilimia 40 zikitengwa kwa mradi huo unaotarajiwa kuanza
Julai.
Dk
Kalemani alisema mkandarasi atafanya kazi za awali kwa miezi mitatu
kabla ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya mradi unaotarajiwa kukamilika
katika kipindi cha miezi 36.
“Fedha
za maendeleo za ndani Sh700 bilioni zimetengwa katika mwaka wa fedha
2018/19 kwa ajili ya kuanza kutekeleza kazi hizo,” alisema.
Alizitaja kazi hizo kuwa ni ujenzi wa kambi na ofisi za wafanyakazi na njia kuu za kupitisha maji.
Dk
Kalemani alisema katika mwaka wa fedha 2017/18, kazi iliyofanyika ni
uchambuzi wa zabuni zilizowasilishwa na makandarasi walioonyesha nia ya
kutekeleza mradi huo.
“Ujenzi
wa njia ya msongo wa KV 33 kutoka Dakawa kwa ajili ya kupeleka umeme
utakaotumiwa na mkandarasi wakati wa ujenzi wa mradi ulianza Novemba
mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu,” alisema.
Mradi huo unatarajiwa kujengwa kwenye eneo la kilomita 1,350 za mraba na litajengwa bwawa lenye urefu wa mita 134.
Kwa
mujibu wa mpango mkuu wa mfumo wa nishati wa mwaka 2016, mahitaji ya
umeme kwa ajili ya viwanda na shughuli za biashara yataongezeka hadi
asilimia 18 kati ya mwaka 2015 na 2020 kutokana na maendeleo ya gesi,
ujenzi wa miundombinu ya usafiri, kuongezeka kwa uwekezaji kutoka nje,
kukua kwa kiwango cha elimu na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano.
Katika
mpango huo wa mwaka 2016, haja ya kuongeza uzalishaji umeme inaonekana
kubwa kutokana na matumizi ya mkaa kufikia asilimia 80 na hivyo mikakati
ya umeme kutarajiwa kupunguza matumizi hadi asilimia 49 ifikapo mwaka
2040.
Hata
hivyo, baadhi ya wabunge wamekuwa wakipinga kuanza kutekelezwa kwa
mradi huo wakitaka kwanza ufanyike upembuzi yakinifu wa athari za
kimazingira kabla ya utekelezaji kuanza, jambo ambalo Serikali imesema
linafanyika na sasa timu yake imeenda eneo hilo kuzungumza na wadau.
Pia
wanaharakati za mazingira wanadai kuwa utekelezaji wa mradi huo
utaondoa hali ya uasilia wa eneo hilo na kusababisha viumbe, mimea na
wananchi kuhamishwa kupisha mradi pamoja na kuathiri shughuli nyingine
za kiuchumi kama utalii.
Lakini
jana, Dk Kalemani alieleza umuhimu wa mradi huo mkubwa wa kuzalisha
umeme akisema miongozi manufaa ya Stiegler’s Gorge ni kuvutia watalii,
hivyo kuongeza fedha za kigeni, kuongezeka kwa shughuli za majini kama
vile michezo ya majini.
Alisema visima 10 ndani ya bwawa vitaongeza mazalia ya samaki, mamba na viboko, hivyo kuvutia watalii.
Waziri
alisema litajengwa tuta la kuzuia maji lenye urefu wa sawa na ghorofa
45 kwenda juu na upana wa kilomita moja litakalovutia utalii na hata
kutumiwa na maharusi walio fungate.
Alisema
manufaa mengine ni pamoja na kutunza maji katika bwawa la mradi
yanayoweza kumwagilia hekta 250,000 za mashamba, hivyo kukuza shughuli
za umwagiliaji. Alisema bwawa hilo litakuwa na ukubwa wa mita za mraba
914.
Pia, kutoa huduma za kijamii katika maeneo ambayo yanazunguka mradi huo ikiwamo wananchi hao kuruhusiwa kufanya uvuvi.
Dk
Kalemani alisema umeme utasambazwa maeneo ya vijiji 49 vya jirani
kutoka wilaya za Morogoro Vijijini, Kibiti, Rufiji, Ulanga, Malinyi na
Mlimba.
Alisema
wananchi hawataondolewa wala kuhamishwa katika makazi yao na Mamlaka ya
Maji Safi na Maji Taka (Dawasa) imeshaanza kufanya utafiti wa mahali
watakapochukua maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani kwa wananchi wa
Pwani na Dar es Salaam.
Katika
mikoa hiyo, alisema maji yatapita katika vijiji vya wilaya za Rufiji,
Kibiti, Mkuranga, Temeke na Kigamboni, hivyo kuingia katika mfumo wa
maji wa Jiji la Dar es Salaam na kutoa ajira kwa watu 10,000.
Dk
Kalemani alisema huo mradi utatoa huduma za kijamii kwa kuchangia
katika ujenzi wa shule, vituo vya afya na viwanja vya michezo katika
kaya zitakaozunguka mradi na wilaya za Malinyi, Ulanga, Morogoro
Vijijini, Kibiti, Rufiji, Mlimba na maeneo mengine ya jirani.
Alisema
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hutoa takriban Sh150 bilioni kwa
mwaka kati ya hizo Sh66 bilioni huelekezwa kwenye huduma za jamii katika
miradi ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji.
Dk
Kalemani alisema mradi utakapokamilika utazalisha Megawati 2,100.
Alisema umeme utakaouzwa kwa wateja utaingiza Sh1.6 trilioni kwa mwaka.
Alisema
kulingana na usanifu, mradi unatarajiwa kudumu kwa miaka 80 tangu
utakapoanza uzalishaji na kwamba, miradi mingine ya Kihansi na Mtera,
uhai wake ni angalau miaka 50.
Kuhusu
mpango wa kutunza mazingira, Dk Kalemani alisema Tanesco itaendelea
kutenga fedha kwa ajili ya uendelezaji mazingira kutokana na athari
zinazoweza kujitokeza.
No comments:
Post a Comment