Mbunge
wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amewaasa wazazi
kushiriki katika kuboresha miundombinu ya shule ili kutengeneza
mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia badala ya kuiachia
Serikali peke yake
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu wa Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la
Ilemela, Ndugu Michael Goyele alipomwakilisha mbunge huyo katika
ufunguzi wa mafunzo ya kujitambua na kushiriki katika kutatua
changamoto zinazowakabili wasichana yanayotolewa na Taasisi isiyo ya
Serikali ya Tanzania Youth Alliance For Development and Cooperation
TYADCO iliyopo jijini Mwanza katika shule ya sekondari Buswelu ambapo
mbali na kuelezea hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuhakikisha
sekta ya Elimu inaimarika ndani ya Jimbo la Ilemela ikiwemo ujenzi wa
mabweni ya wasichana kwa shule ya sekondari Buswelu, ugawaji wa vitabu
kwa baadhi ya shule za Jimbo hilo, ukarabati wa shule kongwe za Bwiru
wasichana na wavulana, ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi
na sekondari kupitia mradi wa ufatuaji tofali unaoendeshwa na taasisi
ya The Angeline Foundation pia amewaasa wazazi kuhakikishia wanaunga
mkono jitihada za serikali katika kuweka mazingira rafiki ya utoaji wa
elimu nchini badala ya kuacha jukumu hilo kwa serikali peke yake jambo
linalochangia kudumaa kwa elimu
‘… Jukumu la kuboresha miundombinu ya shule si la Serikali peke yake,
Ingawa tumekuwa tukiona hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali
kama utoaji wa elimu bure na ugawaji wa vitabu mashuleni lakini na sisi
wazazi tunaowajibu katika kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu kwa
watoto wetu…’ Alisema
Aidha amewaasa wanafunzi kuzingatia masomo na kujiepusha na mazingira
hatarishi yanayokwamisha ufikiaji wa ndoto zao kwa kujiingiza katika
vitendo viovu kama kubeba mimba kabla ya wakati na utumiaji wa madawa
ya kulevya huku akiahidi kompyuta kwa shule ya Buswelu pamoja na
kuwasomesha wanafunzi watakaofanya vizuri katika mtihani wao wa kidato
cha nne mwaka huu kwa kupata daraja la kwanza
Akimkaribisha mgeni rasmi mkurugenzi wa taasisi ya TYADCO Ndugu Aloyce
Masana mbali na kumshukuru Mbunge wa Jimbo hilo kwa kukubali kushiriki
katika ufunguzi huo, amewataka wanafunzi waliohudhuria mafunzo hayo
kuitumia elimu waliyoipata kwa maslahi mapana ya taifa sanjari na
kuzitaka taasisi binafsi kuendelea kuiunga mkono serikali katika kutatua
changamoto za kijamii
Akisoma risala kwa mgeni rasmi, mwanafunzi Sabrina Mohamedi Musa
amezitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili shule yao ikiwa ni pamoja
na idadi ndogo ya walimu wa masomo ya Sayansi, vifaa vya kujifunzia,
maji na mabweni huku akiomba kupatikana ufumbuzi wa haraka ili waweze
kufanya vizuri katika masomo yao
Mafunzo hayo pia yalihusisha taasisi mbalimbali ikiwemo Benki ya NMB,
Benki ya CRDB, Wataalamu kutoka hospitali ya mkoa Mwanza SekeuToure na
Wataalamu wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
19.05.2018





No comments:
Post a Comment