Wanafunzi
wawili wamefariki dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wanatumia kuvuka
kupinduka na kuzama eneo la Chulwi kitongoji cha Tambani Wilaya ya
Mkuranga Mkoa wa Pwani jana Mei 14, 2018. Katika ajali hiyo, watu wanane
waliokolewa.
Mkuu
wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga amesema leo Mei 15, 2018 kuwa
mtumbwi huo ulikuwa na watu 10, wakiwamo wanafunzi hao, kwamba mwili wa
mwanafunzi mmoja umepatikana na mwingine unaendelea kutafutwa.
“Wanafunzi hawa mmoja alikuwa anasoma darasa la awali na mwingine darasa la pili,” amesema Sanga.
Amesema
kutokana na mvua kuendelea kunyesha maeneo mbalimbali wilayani humo,
amezuia wanafunzi kwenda shule kwa kuwa pia mito imejaa maji jambo
linalosababisha uvukaji kuwa mgumu.
Amesema
kuwa mvua hizo zilimfanya ashindwe kufika eneo la tukio jana baada ya
gari yake kukwama na amehakikisha leo kufika maeneo yote ambayo yamepata
madhara ya mvua.
“Leo
nitatembelea maeneo yaliyopata madhara ya mvua eneo la Magawa, Kata ya
Kisiju huko kuna nyumba zimeezuliwa na idadi kamili nitatoa baadaye,”
amesema Sanga.

No comments:
Post a Comment