Katibu
mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema ni ruksa kwa wabunge wao kuikosoa
Serikali, lakini akatoa angalizo; wasitumie lugha kali, wasizushe wala
kutia chumvi mambo wasiyo na uhakika nayo.
Dr Bashiru ameyasema hayo katika mahojiano a gazeti la Mwananchi.
Alisema mbunge atakayeitetea Serikali ya CCM ambayo imewekwa madarakani na wananchi, pia hatakuwa amefanya kosa.
“(Wabunge wa CCM) Waisimamie Serikali na waikosoe kwa ushahidi na kwa hoja, ama hadharani katika Bunge,” alisema Dk Bashiru.
“Lakini kwa kufuata taratibu za kibunge au ndani ya kamati ya wabunge wa CCM.”
Alisema
hiyo ni kwa sababu kamati ya wabunge ina uongozi na taratibu zake na
kwamba katika kamati hiyo wabunge hukosoana waziwazi na kuambiana ukweli
kuliko hata wanavyofanya hadharani.
“Kwa
sababu mbunge wa CCM ana chama chake, ana wapigakura wake, ana haiba
yake mwenyewe na msimamo wake na ana Taifa lake, maeneo haya manne
anahitaji kuyawekea uwiano,” alisema mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Maeneo
haya yana masharti. Huwezi ukawa mbunge unaisifu Serikali inayoelekeza
mambo ambayo yanaharibu uchumi, huo sio utaifa. Ndio maana hata mwalimu
alifikia mahali akasema ‘CCM sio mama yangu. Kama CCM inaweza kuwa na
mambo ya ovyo naweza kuachana nayo’.”
Alisema ndio maana kuna wakati Mwalimu Nyerere alimuunga mkono mgombea wa upinzani.
Alisema
alifanya hivyo kwa sababu alidhani mgombea aliyeteuliwa na CCM hakuwa
anafaa na yule aliyeteuliwa na upinzani alikuwa anafaa.
“Kwa
hiyo mwalimu hapo alikuwa hasaliti chama chake, alikuwa anasimamia
nchi. Huwezi kukubali mtu wa ovyo ashinde kwa sababu ni CCM. Kazi yetu
ndani ya chama ni kuhakikisha tunachuja wagombea wetu ili wale
tunaowatoa wawe wanakubalika,” alisema.
“Na
(wabunge wa CCM) wakishashinda, wanakwenda kujiwakilisha wao wenyewe
kwa nafsi zao kama Watanzania, kukiwakilisha chama, wapigakura ambao ni
wana CCM na wasio wanaCCM na nchi yao,” alisema Dk Bashiru.
Hata hivyo, Bashiru alisema kwa bahati mbaya wabunge wa pande zote mbili wameshindwa kuweka uwiano wa maeneo hayo.
“Wengine
ukiwasikiliza ni porojo zao. Wamedandia hoja fulani lakini wengine
ukiwasikiliza wameegemea kwenye chama zaidi. Lakini msimamo ule una
madhara kwa wapiga kura wake ambao wengine si wanachama wa chama
chochote,” alisema.
Alisema ukisikiliza wabunge wengine, unaona hawana mtazamo wa kitaifa na wanakuwa wanavuta sehemu moja.
“Kwa
hiyo ni kazi ya kuelimishana na tunafanya hivyo kwenye vikao na kwenye
kamati kuhakikisha kuwa wabunge wanatoa michango yao kwa nguvu zao zote,
vipaji vyao vyote, kusimamia maslahi ya nchi yao, maslahi ya chama
wapiga kura wao na taifa,” alisema.
Dk
Bashiru alisema wakipatikana wabunge wa aina hiyo, wanaoangalia maslahi
ya kila upande bila kujali wanatoka kambi gani, Tanzania itakuwa na
Bunge imara la kuisimamia Serikali.
Kuhusu
kuingiliwa uhuru kwa wabunge wa CCM wanapochangia mijadala, Dk Bashiru
alisema wamekubaliana na uongozi wao na wanafanya mpango katika Baraza
la Wawakilishi kuhakikisha kuwa sekretarieti ya chama inafuatilia
mwenendo wa utendaji wa wabunge wa chama hicho katika vikao vya maamuzi.
Alisema
mbunge anayelalamika kuminywa kwa uhuru wake akihisi kamati ya uongozi
wa chama hicho imemnyima uhuru wa kuzungumza katika chombo cha maamuzi,
aende kumueleza.
“Juzijuzi
nimezungumza naye vizuri (mmoja wa wabunge wa CCM) na tutakuja kukutana
naye. Ni kijana ambaye ana mawazo ya kujenga na ana misimamo lakini
tukubaliane kuwa si kila unachokiamini lazima kikubalike katika
mjadala,” alisema Bashiru na kuongeza.
“Kama
mtu mvumilivu lazima ifike mahali ujue kuwa mawazo yatakayotawala
maamuzi, ama yanaweza kuwa sehemu ya mawazo yako au yakatofautiana na
mawazo yako. Kwa hiyo sitarajii kabisa vyombo hivi vikawa na mawazo
yanayofanana.”
Alisema iwapo kuna taratibu ambazo zinawanyima nafasi ya kuzungumza wabunge wa CCM, utaratibu huo hautaruhusiwa.
“Tunahitaji
kamati za wabunge ziwe imara ziwe na mazingira huru ya kukijenga chama
ndani ya Bunge sio kuwaingilia wabunge uhuru wao, lakini ukishakuwa
mwanachama ukubali umeugawa uhuru wako,” alisema.
“Ni
suala la kugawagawa tu. Ni sawa na ndoa, unagawa kidogokidogo. Kama
nilivyosema ni makundi manne hapo. Ni kweli uhuru wa wabunge
umegawanyika na hakuna Bunge duniani ambako utakuta ubunge wao uko
kamili na ukikuta hivyo, hilo halitakuwa Bunge bali ni kundi fulani,”
alisema.
Alisema
Bunge ni lazima litakuwa na utaratibu ambao unamnyang’anya uhuru mbunge
lakini uhuru huo lazima uwe na maslahi kwa Taifa au kwa wapigakura,
mbunge mwenyewe au chama.
“Labda
kama (mbunge) anasema chama kimechukua kipande kikubwa kuliko vingine,
hilo linajadilika. Mimi ningetaka chama kiweke utaratibu wa kuwapa uhuru
wabunge kutumia vyombo hivyo kama kamati za Bunge na kamati ya wabunge
wa CCM kuwa vyombo vya majadiliano na mashauriano,” alisema.
Hata
hivyo, alisema majadiliano yawe ni ya kukosoana lakini wasitumie lugha
kali, wasizushe mambo, wasiweke chumvi kwa jambo ambalo si la kweli na
waibue mambo mapya ya maslahi ya wananchi.
Dk
Bashiru pia alisema si kila kitu kinachozungumzwa kina maslahi na
wananchi na kwamba Afrika haijafikia kiwango cha Bunge linazungumza
masuala ya wananchi wakati wote.
“Sauti ya wananchi haiwezi kusikika kwenye Bunge la kitaifa tu,” alisema.
“Tungeimarisha
vyombo vya vijiji na kuheshimu maamuzi ya vyombo vya serikali za kijiji
na wilaya, matatizo mengi yangesemwa na kutatuliwa na vyombo hivyo.
Wabunge wasisahau tunapoimarisha nguvu ya Bunge lazima tuimarishe vyombo
vingine vya maamuzi vya chini.”
Alisema
demokrasia ya kweli katika nchi masikini kama ya Tanzania ni kuwa
vyombo imara vya maamuzi vya chini ambako ni karibu na wananchi.
“Nenda
kule vijijini ni mikutano mingapi ya vijiji inafanyika? Hakuna
anayeratibu na anayejali lakini ipo kikatiba. Akishachaguliwa, anasubiri
uchaguzi mwingine hakuna anayejali. Tunataka wabunge wetu wasibebe
demokrasia ya kibunge pekee kama ndio demokrasia pekee.”
Pia alisema demokrasia katika ngazi ya vijiji inatakiwa ipate nguvu kwa kuwa ndiko matatizo makubwa.
“Nani anaratibu maoni kwenye mikutano inayofanyika chini ya miti vijijimi na ni nani anasikiliza?” alihoji.
Alisema
CCM inataka kuona vyombo vyote vya maamuzi vinapata nguvu na sauti zake
zisikilizwe, lakini bahati mbaya Bunge ndilo linaonekana ndio chombo
pekee cha uwakilishi.
Alisema
asilimia 70 ya serikali za vijiji na asilimia 65 za serikali za mitaa
na halmashauri zipo chini ya CCM na ndivyo atakavyoshughulika nazo.

No comments:
Post a Comment