Monday, June 4, 2018

JAMII YAASWA KUWAFICHUA NA KUWASAIDIA WALEMAVU

Jamii imeaswa kuwafichua na kuwasaidia watoto walemavu ili waweze kupata huduma muhimu za afya na elimu zitakazowasaidia kufikia ndoto zao
Kauli hiyo imetolewa leo na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza kupitia kundi la vijana (UVCCM) Mhe Maria Kangoye wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa chama cha mapinduzi kata ya Kirumba wilayani Ilemela alipokuwa akikabidhi jumla ya baiskeli 25 kwa walemavu wa mkoa wa Mwanza ambapo ameiasa jamii kutowaficha walemavu na kuwakandamiza katika kutimiza malengo yao.

‘… Imefika hatua tunataka kuliona suala la ulemavu kama jambo la kawaida, tumeshuhudia wakifichwa majumbani, tumeshuhudia wakikosa fursa mbalimbali kutokana na hali zao, wengi wamekuwa hata wakipelekwa mashuleni wanarudishwa …’ Alisema
Aidha Mhe Kangoye amempongeza na kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa namna anavyoshirikiana nae katika kuhakikisha wanawatumikia wananchi kwa kutatua kero zao sambamba na kuwataka wanachama hao kueleza mazuri yanayofanywa na Serikali ya chama cha mapinduzi chini Mhe Rais Dkt John Magufuli  na wasaidizi wake.
Nae Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) wilaya ya Ilemela Ndugu Salome Kipondya amemshukuru mbunge huyo kwa uamuzi wake wa kusaidia watoto walemavu wa wilaya yake huku akimuahidi ushirikiano katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwaletea wananchi maendeleo..

Kwa wilaya ya Ilemela watoto Brenda Kennedy mwenye umri wa miaka 17 anaesoma mpango wa elimu ya watu wazima, Eric Ngembe  mwenye umri wa miaka 14 mkazi wa Kirumba anaesoma Sunrise sekondari na Kelvin Razaro mwenye umri wa miaka 5 mkazi wa Buzuruga anaesoma shule ya awali wamemshukuru mbunge huyo kwa kunufaika na baiskeli hizo za walemavu alizozitoa zitakazowasaidia katika maisha yao ya kila siku.

Zoezi hilo la ugawaji wa baiskeli kwa watoto walemavu lilishuhudiwa pia na mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mwanza, Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela, na madiwani wa viti maalum wa wilaya hiyo.






No comments:

Post a Comment