Monday, June 25, 2018

Rais Magufuli Awalilia Watu 14,waliokufa Kwa Ajali Ya Hiance Iliyogongana Na Lori La Mchanga Mkuranga

Rais Dkt. John Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa ya vifo vya watu 14 waliopoteza maisha baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori la kubebea mchanga katika eneo la Dundani Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.

Dkt. Magufuli amesema hayo katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo baada ya kupita masaa kadhaa tokea ajali hiyo kutokea leo Juni 25, 2018 wakati basi dogo lililowabeba wanafamilia, ndugu na jamaa waliokuwa wakielekea Msata kuhudhuria sherehe za kumaliza mafunzo ya kijeshi  kwa mtoto wao, kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Dundani kuchukua mchanga.

"Naomba unifikishie pole nyingi kwa wanafamilia wote waliopatwa na msiba, waambie naungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao, na sote tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi", amesema Rais Magufuli.


Kwa upande mwingine Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wanne wa ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na majukumu yao ya kila siku.

No comments:

Post a Comment