Jamii imeaswa kuwakumbuka kwa kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi ili kuandaa taifa imara
Kauli hiyo imetolewa leo na diwani wa kata ya Kawekamo manispaa ya Ilemela Mhe Japhes Rwehumbiza wakati wa kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya shule kwa wanafunzi wa shule za msingi Kilimani na Pasiansi ikiwemo madaftari, kalamu na sare za shule vilivyotolewa na kikundi cha Amani kilichopo ndani ya kata hiyo ili kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi ili waweze kusoma na kufikia malengo yao
‘… Ndugu zangu jukumu la kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ni letu sote, kila mmoja ana nafasi yake jamii mna wajibu wenu, viongozi tuna wajibu wetu na wazazi wana wajibu wao, tuendelee kushirikiana katika kusaidia watoto hawa ili kujenga taifa lililoimara …’ Alisema
Aidha Mhe Rwehumbiza amemshukuru mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kutoa tofali zinazotumika katika ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Pasiansi huku akiwataka walimu wa shule hiyo kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu za utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao
Akisoma risala kwa mgeni rasmi ndugu Ndalahwa mbali na kumshukuru Diwani huyo kwa ushirikiano anaotoa kwa kikundi chao, ameomba kufikiriwa kwa kikundi hicho cha Amani katika kunufaika na mkopo unaotolewa na manispaa ya Ilemela ili waweze kuongeza mtaji katika biashara zao sambamba na kutekeleza shughuli za kujikwamua kiuchumi
Kwa upande wake mwanafunzi Saverin Abel anayesoma darasa la saba katika shule ya msingi Pasiansi mbali na kushukuru kwa msaada huo ameomba makundi mengine katika jamii kujitokeza na kuendelea kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kupata elimu bora na kutimiza ndoto zao.
No comments:
Post a Comment