Warimbwende wa shindano la kumsaka mrembo wa mkoa wa Mwanza kwa mwaka 2018 lililopambwa na kauli mbiu ya ‘Urembo na Kazi kwa Maendeleo ya Jamii’ wamejitokeza kumuunga mkono mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kuhamasisha jamii kushiriki katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo zoezi la utoaji bure wa huduma za afya na upimaji wa hiari wa virusi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi linaloendeshwa ndani ya wilaya hiyo kwa kushirikisha madaktari bingwa kutoka nchi ya Marekani, wataalamu wa afya wa manispaa ya Ilemela na Ofisi ya mbunge
Akizungumza wakati wa uhamasishaji jamii juu ya kujitokeza kupima afya zao na kupata huduma za matibabu katika kituo cha afya Buzuruga muandaaji wa shindano la kusaka mrembo wa mkoa wa Mwanza ambae pia ni mkurugenzi wa taasisi ya Mepal Management Bi Pamela Irengo amesema kuwa shindano la kumsaka mrimbwende wa mkoa wa Mwanza linataraji kufanyika siku ya Ijumaa ya Juni 06, 2018 katika ukumbi wa Rock City Mall kwa kushindanisha warimbwende 14 kutoka maeneo tofauti tofauti ya mkoa wa Mwanza, Hivyo warimbwende hao kabla ya kuchuana vikali kunyakua taji la Miss Mwanza wameamua kuunga mkono jitihada za mbunge wa jimbo la Ilemela kwa kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano chini Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa jamii kwa kutembelea Ofisi za manispaa hiyo, kutembelea kituo cha afya vya Buzuruga kuhamasisha upimaji wa virusi vya Ukimwi kwa hiari na kupata matibabu ya magonjwa mbalimbali, kutembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha AIC Tunza Ilemela kisha kutoa msaada wa vyakula na vifaa mbalimbali kwa watoto wa kituo hicho
‘… Tunatambua jitihada kubwa za kuwaletea wananchi maendeleo zinazofanywa na mbunge wa jimbo hili kwa kushirikiana na Serikali,Na sisi kama sehemu ya jamii tumeamua kuunga mkono jitihada hizo kwa kuihamasisha jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo …’ Alisema
Kwa upande wake kiongozi wa kundi la madaktari kutoka nchi ya Marekani, Dkt Krishnansu Tewaru amesema kuwa wamekuwa wakishirikiana na Ilemela katika kutoa huduma za afya kwa nyakati tofauti tofauti lengo likiwa ni kusaidia mapambano dhidi ya magonjwa sugu yakiwemo Kansa yanayoonekana kushika kasi na kuathiri watu wengi hivyo kuiasa jamii kujitokeza kupima afya zao kwa hiari ili waweze kupata matibabu
Akihitimisha mganga mkuu wa wilaya ya Ilemela Daktari Florian Tinuga amewashukuru walimbwende hao kwa uamuzi wao wa kuunga mkono zoezi la utoaji wa huduma za afya bure na upimaji wa hiari wa virusi vya maambukizi ya Ukimwi wanaloliendesha kwani muitikio kwa jamii umekuwa ni wa kusuasua hivyo ushiriki wao katika kuihamasisha jamii unaweza kuwa mwarobaini wa kufanikisha zoezi hilo huku akiwatakia heri washiriki wa shindano hilo.
Ikumbukwe kuwa kituo cha afya Buzuruga kinaendelea na ujenzi wa jengo la utawala na maabara kwa ufadhili wa taasisi ya The Angeline Foundation iliyoasisiwa na mbunge wa jimbo hilo, serikali, nguvu za wananchi huku diwani wa kata hiyo Mhe Richard Machemba akishiriki muda wote katika zoezi la upimaji na utoaji tiba linaloendelea ndani ya kata yake.
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga '
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
04.07.2018
No comments:
Post a Comment