Thursday, August 16, 2018

MASHINDANO YA ANGELINE JIMBO CUP 2018 YAZIDI KUSHIKA KASI

Mashindano ya mpira wa miguu ya Angeline Jimbo Cup 2018 yamezidi kushika kasi ambapo siku ya leo Agosti 15, 2018 timu sita zimemenyana vikali katika viwanja vitatu tofauti kikiwemo Kiwanja cha  Shule ya msingi Buswelu, Kiwanja cha Sabasaba na Kiwanja cha Kona ya Bwiru.

Katika kiwanja cha Kona ya Bwiru, Timu ya Kata ya Kirumba imetoka kifua mbele kwa kuitandika Timu ya Kata ya Nyamanoro goli moja kwa sifuri lililofungwa na mchezaji wake jezi nambari Saba aliyejulikana kwa jina la Boniphace Katengasi dakika ya 51 wakati wa kipindi cha pili cha mchezo huo ambapo mpaka mchezo unamalizika matokeo yakisalia kuwa goli moja kwa sifuri huku Goli kipa wa Timu ya Kata ya Nyamanoro akiambulia kadi nyekundu mara baada ya kukiuka sheria za mpira wa miguu kwa kumpiga muamuzi wa mchezo huo.

Akizungumza baada ya kuisha kwa mchezo huo Diwani wa kata ya Kirumba Mhe Alex Ngusa amemshukuru mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kuasisi mashindano hayo yenye lengo la kuibua vipaji huku akitamba kuwa Timu yake itaendelea kufanya vizuri katika mechi zijazo ili kuendelea kuwa Tanuru katika kuoka wachezaji wapya watakaokuwa tegemezi kwa vilabu mbalimbali nchini na taifa kwa ujumla wake.

Katika Kiwanja cha Sabasaba, Timu ya Kata ya Ilemela imeendelea kugawa dozi  kwa awamu hii ikiitandika vikali Timu ya Kata ya Kiseke magoli mawili, La kwanza likifungwa na mchezaji wake Joseph John dakika ya Sita kipindi cha Kwanza kabla ya Timu ya Kiseke kurudisha goli hilo kupitia kwa mchezaji wake Edwin Robert dakika ya Kumi na mbili, Na dakika ya Thelathini na mbili kipindi hicho hicho cha kwanza ndipo mchezaji Emanuel Samuel alipoiongezea Timu yake ya Ilemela goli la pili na kupelekea mchezo huo kuhitimishwa kwa ushindi wa magoli mawili kwa goli moja.

Nae Diwani wa kata ya Ilemela Mhe Wilbard Kilenzi ameisifu Timu yake kwa mchezo mzuri inaoucheza huku akiwaomba wachezaji kujituma zaidi sambamba na wapenzi wa timu hiyo kuendelea kuiunga mkono ili iweze kuwa bingwa wa mashindano hayo.

Wakati huo huo Timu ya Kata ya Buswelu imepimana nguvu na Timu ya Kata ya Mecco mchezo huo ukiisha bila kufungana.  

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga






No comments:

Post a Comment