Jumla
ya miradi 36 yenye thamani ya shilingi bilioni 8.4 iliyopo katika
Halmashauri sita za Mkoa wa Simiyu itapitiwa na Mwenge wa Uhuru ambao
umeanza rasmi mbio zake mkoani humo, Agosti 15, 2018.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka wakati akisoma
salamu za mkoa wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika Kijiji cha
bukundi wilayani Meatu ukitokea wilaya ya Mkalama Mkoani Singida Agosti
14, 2018.
Mtaka
amesema kuwa miradi hiyo inayotarajiwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru ni
kutoka katika Idara ya Elimu, Afya, Maji, Viwanda, Kilimo, Maliasili,
Barabara,Utawala, Sekta binafsi na Vijana na Wanawake.
Akizungumzia
Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 ambao umejikita zaidi katika Elimu
kwa kauli Mbiu “ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA; WEKEZA SASA KWA MAENDELEO
YA TAIFA LETU” amesema, Elimu ni kipaumbele cha kwanza kwa mkoa huo,
ambapo wameweka mikakati mbalimbali ya kuinua elimu na ujenzi wa
miundombinu ya elimu.
“
Simiyu ni mkoa pekee ambao wanafunzi wa madarasa ya mitihani wanakaa
katika kambi za kitaaluma, pia ufaulu wa wanafunzi wetu umeongezeka
mfano, mwaka 2017 mkoa wa Simiyu ulikuwa wa 26 Kitaifa kati ya mikoa 31
lakini mwaka 2018 mkoa umeshika nafasi ya 10 katika matokeo ya kidato
cha Sita” alisema.
Aidha,
Mtaka amesema Simiyu inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa
kushirikisha jamii na wadau mbalimbali ikiwa na mkakati wa kujenga shule
tatu ambazo ni Shule ya Sekondari ya Ufundi Simiyu, Shule ya Sekondari
ya Wasichana na Shule ya Sekondari ya Wavulana.
Hata
hivyo Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Meatu umepita katika miradi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa vyumba vya madarasa katika shule
shikizi ya Mwanyahina, Mradi wenye majengo manne katika Hospitali ya
Wilaya; (jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, maabara na nyumba
ya mtumishi), mradi wa ujenzi wa mahakama ya mwanzo Itinje na mradi wa
ushonaji wa wanawake wa Kijiji cha Mwamishali.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti katika miradi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru,
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles
Francis Kabeho amewataka viongozi na watendaji kusimamia miradi ya
maendeleo kwa weledi na kuhakikisha inatekelezwa kwa wakati kwa viwango
vinavyohitajika na kuzingatia thamani ya fedha(value for maoney) ili
wananchi wapate huduma.
“Utawala
wa Awamu ya tano unataka watu wafanye kazi na kuwajibika
kweli,tunaposema HAPA KAZI TU Mhe. Rais anamaanisha, tukisimamia miradi
kwa ulegelege hatutaweza kufika, inawezekana hata kuchelewa kwa miradi
ni kwa sababu watu wanataka maslahi yao na kusababisha huduma za kijamii
zinakwama ili wao wanufaike, watendaji wa aina hiyo awamu ya tano
hatuwahitaji” alisema Kabeho
Kwa
upande wake mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani akizungumza
mara baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kuweka jiwe
la msingi mradi wa madarasa ya shule shikizi ya Mwanyahina amesema
Viongozi wa wilaya watasimamia ujenzi wa mradi huo na kuhakikisha
unajengwa kwa viwango na kwa wakati ili shule hiyo iwanufaishe wananchi
wa vijiji jirani vinavyoizunguka.
Mwenge
wa Uhuru umeanza mbio zake mkoani Simiyu katika Wilaya ya Meatu Agosti
14, 2018, Agosti 15 utakuwa halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Agosti 16
Halmashauri ya mji wa Bariadi, Agosti 17 Halmashauri ya Wilaya ya
Bariadi, Agosti 18 Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Agosti 19
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na tarehe Agosti 20, utakabidhiwa mkoani
Shinyanga.
No comments:
Post a Comment