Wednesday, August 15, 2018

TIMU YA KATA YA IBUNGILO YAICHAPA KATA YA PASIANSI MASHINDANO YA ANGELINE JIMBO CUP 2018

Mashindano ya mpira wa miguu ya Angeline Jimbo Cup 2018 yameendelea kushika kasi ambapo mechi nne zimechezwa siku ya leo katika viwanja vinne tofauti, Kiwanja cha Sabasaba Timu ya Kata Kawekamo wamechuana vikali na Timu ya Kata ya Nyasaka, Kiwanja cha Bugogwa shule ya msingi Timu ya Kata ya Kayenze imekabana koo na Timu ya Kata ya Shibula, Kiwanja cha Buswelu Timu ya Nyakato imepambana na Timu ya kata Kahama huku Kiwanja cha Kona ya Bwiru Timu ya Ibungilo ikikutana na Timu ya Kata ya  Pasiansi.

Katika kiwanja cha Kona ya Bwiru wenyeji Timu ya kata ya Ibungilo wametoka kifua mbele dhidi ya Timu ya kata ya Pasiansi kwa kuifunga magoli matatu kwa goli moja, Goli la kwanza likiwekwa wavuni na mchezaji aliyejulikana kwa jina la Michael George mwenye jezi nambari 12 dakika ya 74 kabla ya mchezaji Said Said mwenye jezi nambari 15 kuiongezea timu yake hiyo magoli mawili mfululizo dakika 74 na dakika 87 yakiwa magoli ya kusawazisha baada ya timu hiyo kufungwa goli moja katika kipindi cha kwanza dakika ya 45 na mchezaji Peter Timoth wa Timu ya kata Pasiansi.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo Diwani wa Kata ya Pasiansi Mhe Rosemary Mayunga amesema kuwa Timu ya kata yake imeshindwa kufanya vizuri katika mechi hiyo licha ya kujiandaa vizuri kutokana na miundombinu isiyo rafiki ya kiwanja hicho na kuomba mechi itakayofuata ipangwe kiwanja tofauti na hicho ili kuwepo ushindani sawa.

Kwa upande wake mchezaji wa Timu ya Kata Ibungilo Ndugu Tete Jandwa amesema kuwa matokeo walioyapata yametokana na kuzingatia maelekezo kutoka kwa mwalimu wao wa Timu pamoja na mabadiliko aliyoyafanya mwalimu hayo mapema mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili huku akiwahakikishia mashabiki wa Timu hiyo kuendelea kufanya vizuri zaidi ili kukata kiu ya muda mrefu waliyonayo ya kuhakikisha wananyakua kombe la mashindano hayo kwa mwaka huu baada ya kulikosa mwaka uliopita wa mashindano kwa kushika  nafasi ya pili.

Mara baada ya mchezo huu wa leo, Timu ya Ibungilo inataraji kukutana na Timu ya kata Kitangiri katika mchezo ujao utakaochezwa Agosti 16, 2018

‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'







No comments:

Post a Comment