Tuesday, August 21, 2018

SANGABUYE NA SHIBULA ZATUNISHIANA MISULI ANGELINE JIMBO CUP 2018



Timu ya Kata ya Sangabuye na Timu ya Kata ya Shibula zimetunishiana misuli kwa kutoka sare ya bila kufungana katika mechi ya mwisho ya mzunguko wa kundi D  iliyochezwa katika uwanja wa shule ya msingi Bugogwa kata ya Bugogwa.

Akizungumza mara baada ya kuisha kwa mchezo huo, Diwani wa kata ya Shibula Mhe Swila Dede mbali na kuipongeza Timu ya kata yake kwa matokeo waliyoyapata, amewaasa wachezaji wa Timu hiyo kuyatumia mashindano ya Angeline Jimbo Cup 2018 kama sehemu ya kuonyesha uwezo wao kitendo kitakachowasaidia kuonwa na Vilabu vikubwa na  kusajiliwa.

Nae katibu wa umoja wa vijana kata ya Sangabuye Ndugu Daniel Lupemba ambae pia ndio Kocha wa timu hiyo, amewataka wachezaji wake kutokata tamaa kwa matokeo waliyoyapata pamoja na kuwaomba mashabiki wao kuendelea kuwaunga mkono.

Wakati huo huo mchezo uliochezwa katika kiwanja cha Buswelu ukikutanisha Timu ya kata ya Nyakato na Timu ya kata ya Nyamhongolo umeisha kwa Timu hizo kutoka sare ya kufungana magoli matatu kwa matatu huku ukitawaliwa na ushindani mkubwa baina ya Timu hizo mbili zilizokuwa zimekamiana vikali.

Katika kiwanja cha Sabasaba,  Timu ya kata ya Kawekamo imekutana na Timu ya Kata ya Ilemela ambapo mchezo huo umeisha kwa kufungana goli moja kwa moja, Goli la Timu ya kata ya Kawekamo likifungwa dakika ya 10 katika kipindi cha kwanza na mchezaji wake Yona Ndabira mwenye jezi namba 8, huku Goli la kusawazisha la Timu ya kata ya Ilemela likifungwa na mchezaji Emanuel Frank mwenye jezi namba 8 katika kipindi cha pili.

Diwani wa kata ya Kawekamo Mhe Japhes Rwehumbiza amemshukuru mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kuasisi mashindano hayo huku akitamba timu ya kata yake kuchukua ubingwa wa mashindano hayo kwa mwaka huu wa 2018 kwa kuwa ana kikosi kizuri chenye uzoefu na mashindano hayo.

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’










No comments:

Post a Comment