Monday, September 3, 2018

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AMPONGEZA DKT ANGELINE MABULA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa Ndugu Charles Kabeho amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa ushiriki wake katika kuchangia, kusimamia na kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya jimbo lake wakati wa sherehe za kuulaki Mwenge wa Uhuru wilayani humo uliopambwa na kauli mbiu ‘Wekeza katika Elimu kwa Maendeleo Endelevu’.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kayenze ndogo, kata ya Bugogwa wilaya ya Ilemela mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya msingi Bugogwa ‘B’ iliyojengwa kwa ushirikiano wa wananchi, serikali na viongozi wao  huku akiwaasa wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani kuendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli za kujiletea maendeleo sambamba na kueleza azma ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli katika kupambana na Umasikini, Rushwa, Maradhi ya Ukimwi na Malaria.

‘… Nitumie nafasi hii kumpongeza mbunge wa jimbo la Ilemela, mstahiki meya na madiwani wake kwa kuchangia, kusimamia na kuhamasisha utekelezaji wa miradi hii ya maendeleo, Ninaamini bila usimamizi mzuri miradi hii isingefika hapa …’ Alisema   

Aidha Ndugu Kabeho amemuasa mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa barabara ya Kitangiri-Kabuhoro na mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa mizani uliopo kata ya Kirumba kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuzingatia ubora unaotakiwa.

Kwa upande wake mkimbiza Mwenge kitaifa Ndugu Issa Abbas kutoka Tanzania Visiwani mbali na kuwakumbusha wazazi juu ya kutosahau wajibu wao katika kumpatia mtoto Elimu bora mara baada ya Serikali kufuta michango yote iliyokuwa Kero, ameelezea historia ya Mbio za Mwenge huku akisisitiza kuwa Mwenge huo wa Uhuru hauna itikadi yeyote ya Kichama, Kidini wala Kikabila.

Nae Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Magufuli, amemshukuru kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge na wenzake alioambatana nao kwa kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Jimbo lake sambamba na kuwaomba wanancnhi na viongozi wenzake kuzidi kushiririkiana katika kuwaletea wananchi hao maendeleo.      

Miradi iliyofunguliwa, kuwekwa jiwe la msingi na kuzinduliwa na Mwenge huo ndani ya wilaya ya Ilemela ni pamoja na Ufunguzi wa karakana ya mafunzo ya ufundi umeme wa viwandani katika chuo cha VETA uliogharimu milioni 320,398,091.27, Ufunguzi wa Bweni la Wasichana Shule ya Sekondari Buswelu uliogharimu milioni 150,888,910, Uwekaji wa Jiwe la msingi Zahanati ya Lukobe uliogharimu milioni 46,615,000, Ujenzi wa shule ya msingi Bugogwa B uliogharimu  milioni 50,189,000,  ujenzi wa barabara ya Kabuhoro-Ziwani yenye urefu wa Km 1.5 kwa  kiwango cha Lami uliogharimu milioni 916,812,210, mradi wa Mzani wa kupima mazao ya Samaki uliopo kata ya Kirumba    na mradi wa kituo cha kupambana na kudhibiti matumizi ya madawa ya kulevya Sober House.                             

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'

Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
03.08.2018










No comments:

Post a Comment