Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angline Mabula amefungua mkutano wa Injili unaoendeshwa na Kanisa la Africa Inland Church katika viwanja vya Shule ya Msingi Bugogwa kuanzia Agosti 29-02, 2018 ukikutanisha kwaya nne za AIC Mwanza Town, AIC Dar es Salaam, AIC Neema Nairobi na AIC Naisambu ya Kitale Eldoret.
Akifungua mkutano huo Mhe Dkt Angeline Mabula amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa Kanisa katika kuleta maendeleo na kuwahakikishia kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli itaendelea kushirikiana na kanisa huku akiwaasa waumini wa dini zote nchini kuithamini, kuitunza na kuilinda amani iliyoasisiwa na waasisi wa taifa la Tanzania na nchi ya Kenya sambamba na kuwaombea viongozi wa mataifa hayo mawili kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo, kupambana na rushwa, kusimamia rasilimali za nchi na kusimamia uwajibikaji katika utumishi wa umma
‘.. Serikali inatambua mchango wa kanisa katika nchi, hivyo nawaomba tuendelee kushirikiana kuihamasisha jamii juu ya kuitunza na kuilinda amani yetu tuliyonayo, Pasipo na amani hakuna maendeleo ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amekemea vitendo viovu katika jamii vikiwemo ubakaji, ujambazi, mimba za utotoni, mauaji ya albino, wizi, unyang’anyi, unyanyasaji wa kijinsia na ukandamizaji na kuitaka jamii kuungana na Serikali katika kupiga vita vitendo vya namna hiyo ili kujenga jamii iliyosawa na yenye haki.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Bi. Emma Mashauri ametaja malengo ya kufanya mkutano huo ikiwemo kuikumbusha jamii juu ya kumrudia Mungu ili kupunguza matendo yasiyo na utu, kuwarudisha kundini wale waliokata tamaa na kurudi nyuma kiimani, kuhimiza matendo mema na yanayokubalika katika jamii na kukemea matendo yote yanayoiondoa jamii katika amani.
Kwa upande wake kiongozi wa Kanisa hilo na Mchungaji mwenyeji kutoka Pastoreti ya Igombe, Mchungaji Nikodemo Mahona amemshukuru mbunge huyo kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kujumuika pamoja nao katika ufunguzi huo licha ya kuwa na majukumu mengi na makubwa ya ujenzi wa taifa.
Ufunguzi wa mkutano huo wa Injili ulihudhuriwa pia na Diwani wa Kata ya Bugogwa Mhe Wlliam Mashamba, Mchungaji John Kamoyo kutoka Dar es salaam, Mchungaji kutoka Naisamu, Mchungaji kutoka Nairobi, Mchungaji kutoka Shinyanga na kuhitimishwa kwa ibada fupi ya kuombea mataifa ya Tanzania na Kenya na viongozi wao kama ishara ya kutambua kazi kubwa wanayoifanya.
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela







No comments:
Post a Comment