Thursday, August 30, 2018

MBUNGE WA JIMBO LA ILEMELA AKABIDHI SAMANI ZA OFISINI KWA KILIMANI SEKONDARI.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ametekeleza ahadi yake ya kusaidia Samani za Ofisini (Viti na Meza) kwa Shule ya Sekondri Kilimani iliyopo Kata ya Kawekamo wilaya ya Ilemela ikiwa ni muendelezo wa juhudi zake za kuhakikisha anaboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kuinua kiwango cha taaluma jimboni humo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo kwa niaba ya Mbunge huyo, Katibu wa Ofisi ya Mbunge Kanda ya Kirumba Mhe Fatuma Kaloli amesema kuwa, Mbunge anatambua mchango wa walimu katika jamii hasa katika kuandaa wataalamu wanaotegemewa na Serikali ili kufikia uchumi wa Viwanda, hivyo kuwaomba kuwa wavumilivu na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili

‘… Mbunge anatambua mchango wenu, Hiki alichokifanya leo ni kudhihirisha kuwa yupo pamoja na nyie katika kumaliza changamoto zinazowakabili, Inawezekana tusizimalize zote kwa wakati mmoja lakini tukiendelea kushirikiana na kuungana mkono kwa maana ya Serikali,  Viongozi na Wananchi kwa pamoja ninaamini nyingi zitapungua …’ Alisema

Aidha Bi. Fatuma Kaloli  amewaasa walimu wa shule hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sheria za utumishi wa Umma ili kujiepusha na vitendo visivyofaa vitakavyochangia kudumaa kwa Elimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Kilimani Mwalimu Kicheta amemshukuru mbunge huyo kwa kutambua adha iliyokuwa ikiwakabili ya upungufu wa Samani za ofisini na kuamua kuitatua huku akimuomba kuendelea na moyo huo wa kutatua changamoto nyenginezo sambamba na kumhakikishia ushirikiano kwa lengo la kuinua taaluma jimboni humo.

Akihitimisha makabidhiano hayo, Diwani wa Kata ya Kawekamo Mhe Japhes Rwehumbiza pia amemshukuru mbunge huyo kwa jitihada zake za kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa kata yake, huku akiwaomba watumishi na wananchi kwa umoja wao kuendelea kushirikiana na viongozi wao ili kujiletea maendeleo.

Baada ya makabidhiano hayo, Viongozi hao wamepata fursa ya kuitembelea shule ya Sekondari Pasiansi kwa lengo la  kuzungumza na walimu pamoja na wanafunzi wao, kukagua miundombinu ya shule na mzingira yake kwa ujumla kisha kuahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zilizoibuliwa kupitia ziara hiyo. 

‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’

Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
30.08.2018







No comments:

Post a Comment