Sunday, August 26, 2018

MASHINDANO YA ANGELINE JIMBO CUP 2018 YAJA NA NEEMA YA MABORESHO YA VIWANJA VYA MICHEZO.

Mashindano ya mpira wa miguu kwa Jimbo la Ilemela yanayojulikana kama Angeline Jimbo Cup 2018 yamekuja na neema ya maboresho ya viwanja vya michezo vilivyomo ndani ya Jimbo hilo.

Akizungumza wakati wa zoezi la ukarabati wa uwanja wa mpira wa miguu wa Magomeni uliopo kata ya Kirumba, moja kati ya viongozi wanaoratibu  mashindano hayo ambae pia ni katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wilaya ya Ilemela Comrade Denis Kankono amesema kuwa zoezi la ukarabati wa kiwanja hicho ni matokeo ya jitihada za mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kupitia Mashindano ya Angeline Jimbo Cup 2018 baada ya kilio cha muda mrefu kutoka kwa wananchi wanaotumia kiwanja hicho kwa shughuli za kimichezo

'.. Matengenezo ya kiwanja hiki ni jitihada za mbunge wa Jimbo la Ilemela kupitia Mashindano yake ya Jimbo Cup yenye lengo la kuibua vipaji na kuvikuza ..' Alisema

Aidha kiongozi huyo amewataka wachezaji na wananchi wanaoishi jirani na kiwanja hicho kuhakikisha wanakitunza na kukilinda kiwanja hicho chenye historia kubwa ya kuzalisha wachezaji wakongwe na maarufu wanaocheza timu mbalimbali nchini ili kiweze kutumika na vizazi vijavyo.

Kwa upande wake mhandisi kutoka wakala wa barabara manispaa ya Ilemela (TARURA) aliyekuwa akisimamia zoezi hilo Ndugu Nickson Richard amesema kuwa zoezi la ukarabati wa kiwanja hicho umekuja kufuatia ombi la mbunge wa Jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula katika ofisi yao na kuongeza kuwa zoezi hilo litahusisha pia na viwanja vyengine vya maeneo ya Buswelu na National kwa kadri itakavyowezekana.

Wakati huo huo, Mashindano ya Angeline Jimbo Cup 2018 yamehitimisha hatua ya mzunguko wa kwanza ambapo katika kundi A Timu ya kata ya Ibungilo na Timu ya kata ya Kirumba zimefanikiwa kuingia hatua ya robo fainali, Na kwa kundi B Timu ya kata ya Mecco pekee ikifanikiwa kuingia  hatua ya robo fainali huku Timu ya Kata ya Buswelu na Timu ya kata ya Nyakato zikisubiria kurudia kwa mechi yao kumpata mwakilishi mmoja kuendelea na hatua hiyo baada ya kufanana kwa matokeo ya timu zote mbili, Katika kundi C Timu ya kata ya Ilemela na Timu ya kata ya Kawekamo zimefanikiwa kuingia hatua ya robo fainali, Na kwa kundi D ni Timu ya kata ya Shibula pekee ikivuka hatua hiyo, wakati Timu ya kata ya Bugogwa na Timu ya kata ya Sangabuye zikisubiria maamuzi ya rufaa yao waliyoikata ili kupata timu moja itakayounga na Timu ya kata ya Shibula  kuendelea na hatua ya robo fainali.

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
24.08.2018









No comments:

Post a Comment