Saturday, October 6, 2018

NGELEJA AKAMILISHA ZIARA SENGEREMA

Leo Oktoba 6, 2018, Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mhe William Mganga Ngeleja almaarufu kama "Mtambo wa Maendeleo Sengerema", amehitimisha ziara ya kutembelea vijiji vyote vya jimbo lake la Sengerema kwa mwaka 2018. Ngeleja ambaye amejiwekea utaratibu wa kutembelea kila kijiji kwa kila mwaka leo amehitimisha ziara hiyo kwenye vijiji vya Kata ya Nyampande ambavyo ni Kawekamo, Bugeshi, Nyansenga na Nyampande.

Ziara aliyohitimisha leo Bw Ngeleja ilianza tarehe 23/09/2018 alipofanya mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Pambalu S/Msingi, kata ya Ibisabageni, mjini Sengerema. 

Baada ya Kata ya Ibisabageni Ngeleja aliendelea kuchanja mbuga kwenye vijiji vyote vya kata za Nyamatongo, Ngoma, Chifunfu, Kasenyi, Kasungamile, Kahumulo, Katunguru, Sima, Nyamizeze, Nyamazugo, Buzilasoga, Ibondo, Mission, na hatimaye Nyampande alipohitimishia leo.

Katika ziara hii ambayo Mhe Ngeleja kwa wastani alikuwa akifanya mikutano ya hadhara minne kwa siku amekuwa akiambatana na Uongozi wa CCM Wilaya (Kamati ya Siasa), Watendaji, Wataalam wa Idara mbalimbali za Serikali,  Waandishi wa Habari, na mimi Mjumbe wa Baraza la UVCCM Taifa.

Utaratibu wa Mhe Ngeleja kuendesha mikutano yake ya hadhara umekuwa ukikonga nyoyo za wapiga kura wake. Kwa kawaida kabla ya Ngeleja kuhutubia, yeye hupendelea asomewe taarifa ya Kijiji kwanza ambayo huelezea utekelezaji wa miradi mbali mbali na changamoto zinazowakabili wanakijiji. Akimaliza kuhutubia Ngeleja hukaribisha maswali kutoka kwa wananchi. Kitendo hiki cha kukaribisha maswali huwafurahisha sana wananchi.

Kimsingi hotuba za Ngeleja zimekuwa zikijielekeza kwenye utatuzi wa kero za maji, barabara, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, miundombinu ya elimu, ujenzi wa ofisi za serikali za vijiji, nyumba za watumishi, kilimo, uvuvi, ufugaji, umeme, n.k. Aidha, kupitia Mfuko wa Jimbo, Ngeleja amekuwa akichangia vifaa vya ujenzi kama saruji, mabati, mbao, misumari, n.k, pamoja na kutoa mafuta ya dizeli kwa ajili ya greda la halmashauri ya Sengerema ambalo hutumika kuboresha barabara ambazo haziko Tanroads wala Tarura.

Katika ziara hii Ngeleja aliwajulisha wananchi wake kuhusu miradi mbali mbali ambayo jimbo lake limepata kutoka serikali kuu, mfano mradi mkubwa wa maji unaohusu kata zote zinazopakana na ziwa victoria. Kata hizi ni Kasenyi, Chifunfu, Katunguru, Nyamatongo, Ngoma, Kahumulo, Busisi, Buyagu, na Igalula. Vijiji vyote vya kata hizi vitapata maji safi na salama ya bomba kutoka ziwa victoria. Maandalizi ya mradi huu yanaendelea. 

Pia Ngeleja amewajulisha wananchi wake kwamba vijiji vyote vya Kata za Nyampande na Sima pamoja na kijiji cha Tunyenye navyo vitapatiwa maji safi na salama kutoka mjini Sengerema.

Kuhusu barabara, Ngeleja amewajulisha wapiga kura wenzake kwamba maandaliza ya ujenzi wa lami kwa barabara za Kamanga - Sengerema, Katunguru Nyamazugo na Sengerema - Nyehunge yanakwenda vizuri. Na pia kutajengwa gati la feri ya Serikali kwenye kivuko cha Kamanga. Zaidi ya hapo Ngeleja kawajulisha wananchi kwamba barabara za Sima - Ikoni na ile ya Sengerema - Nyanchenche - Igalula zimepandishwa hadhi na sasa zinahudumiwa na Tanroads.

Aidha Tarura Mkoa wa Mwanza wanakamilisha mchakato wa kuwapata wakandarasi watakaotengeneza barabara za jimbo la Sengerema.

Kuhusu umeme, Ngeleja kawajulisha wananchi kwamba mkandarasi aliyeshinda tenda ya kusambaza umeme jimboni Sengerema tayari ameisharipoti jimboni, hivyo wakati wowote ataanza kazi.

Mwisho lakini si kwa umuhimu Ngeleja amekuwa akiwashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata jimboni kwake, na kwa namna wananchi walivyo na hamasa kushiriki ujenzi wa miradi mbalimbali kwenye maeneo yao.

Nikiwa kama mmojawapo 
wa wana msafara wa Mhe Ngeleja nakiri na kushuhudia kwamba Ngeleja yuko sawa na anakubalika sana kwa wana jimbo lake. Nimeshuhudia mara nyingi kwenye mikutano ya hadhara wananchi wakimpongeza Ngeleja kwa kazi nzuri na kumuomba aendelee kugombea kwa sababu wao wako tayari kuendelea kumpigia kura.

Ama hakika Ngeleja ni Mtambo wa Maendeleo Jimbo la Sengerema.

Kashilimu Juma Richard

Mjumbe wa Baraza  Kuu la UVCCM  Taifa.
0755090711

Ziarani Sengerema

No comments:

Post a Comment