WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema kwamba nchini Tanzania hakuna ubanaji wa
uhuru wa vyombo vya habari wala taasisi zisizo za kiserikali.
Amesema
jambo hilo linadhihirishwa na uwepo wa jumla ya vituo vya redio 152,
ambavyo kati yake ni vituo vitatu tu ndivyo vinavyomilikiwa na Serikali.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Oktoba 24, 2018) katika
maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye viwanja vya
Karimjee jijini Dar es Salaam.
“Tunapenda
kuwahakikishia kuwa, Serikali ya Tanzania inaongozwa na katiba na
sheria za nchi ambazo zinatoa uhuru wa kujieleza na kupata habari,”
amesisitiza.
Waziri
Mkuu amesisitiza kwamba mwananchi yeyote atakayeenda kinyume na sheria,
Serikali itamuwajibisha kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Amesema Serikali imeridhia mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na ule wa haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
Sambamba
na kusimamia haki hizo, Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wake
katika kuiwezesha jamii kuishi salama kwa amani na utulivu kwa
kuzingatia sheria za nchi.
Amesema
kukuza, kuimarisha na kulinda haki za binadamu ni wajibu wa Serikali na
kwa kuzingatia umuhimu huo mwaka 1984 iliingiza sheria ya haki za
binadamu katika katiba.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa zoezi la kuwarejesha wakimbizi
wa Burundi nchini kwao lilikuwa ni la hiari na limetekelezwa baada ya
hali ya amani kurejea.
Amesema
hakuna sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi ambao kwa hiari yao
wameamua kurejea nchini kwao ili wakaendelee na shughuli za kulijenga
Taifa lao.
“Nasisitiza
kuwa zoezi hili ni la hiari. Tangu mwezi Septemba mwaka jana, Tanzania
kwa kushirikiana na Serikali ya Burundi na UNHCR imekuwa ikiwarejesha
wakimbizi hao kwao.”
Amesema
zoezi hilo limekuwa likifanyika kwa kuzingatia usalama na utu wa
wakimbizi hao. Wakimbizi 52,283 wa Burundi wamerejea nchini kwao kati
81,281 waliokwisha jiandikisha.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo baada Serikali kupokea shutuma katika siku za hivi
karibuni kutoka kwa baadhi ya jamuiya ya kimataifa kuhusu uendeshaji wa
zoezi hilo.
Hivyo,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa na
washirika wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa
mujibu wa mkataba wa UN wa mwaka 1967 wa kuwahudumia wakimbizi ili
kufanikisha zoezi hilo la kuwarejesha makwao kwa hiari na kwa kuzingatia
misingi ya haki za binadamu.
Maadhimisho
hayo ya siku ya Umoja wa Mataifa ambao umetimiza miaka 73 tangu
uanzishwe yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.
Wengine
ni Mratibu wa Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bw. Alvaro Rodrigues
pamoja na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 24, 2018.

No comments:
Post a Comment