Mtihani
wa taifa wa kidato cha nne unaanza leo, huku Baraza la Taifa la
Mitihani (Necta) likitoa onyo kali kwa watakaobainika kujihusisha na
vitendo vya udanganyifu.
Baraza
hilo limesisitiza kuwa halitasita kukifutia matokeo kituo chochote cha
mtihani ambacho kitabainika kujihusisha na udanganyifu.
Hayo
yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk.
Charles Msonde, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na
mtihani huo ambao utawahusisha jumla ya watahiniwa 427,181.
Dk.
Msonde alisema baraza linazitaka kamati za mitihani za mkoa,
halmashauri kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya
taifa zinazingatiwa ipasavyo.
“Kamati
zihakikishe kuwa mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na
kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu,”
alisema.
Alisema
wasimamizi wote wanatakiwa kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa
hali ya juu. Wasimamizi wanaaswa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu
kwani baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika
kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani ya taifa.
Dk.
Msonde alisema kwa upande wa wanafunzi, baraza linaamini kuwa walimu
wamewaandaa vizuri katika kipindi cha miaka minne ya elimu ya sekondari.
“Matarajio
ya Baraza la Mtihani ni kuwa wanafunzi watafanya mitihani yao kwa
kuzingatia kanuni za mitihani. Watahiniwa wote watambue kuwa kukiuka
kanuni za mitihani au kufanya udanganyifu kutawafanya wafutiwe matokeo
yao yote,” alisema.
Alisema
baraza linawataka wamiliki wa shule wote kutambua kuwa shule zao ni
vituo maalum vya mitihani, hivyo hawatakiwi kuingilia majukumu ya
wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyaji wa mtihani huo.
Dk.
Msonde alisema hawatasita kukifutia matokeo kituo chochote cha mtihani
endapo baraza litajiridhisha kuwapo na uhatarishi wa usalama wa mitihani
ya taifa.
Aidha,
alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha
mitihani ya kidato cha nne inafanyika kwa maarifa, amani na utulivu.
“Wananchi
wanaobwa kuheshimu eneo la mitihani na kuhakikisha kuwa hakuna mtu
yeyote asiyehusika na mitihani anayeingia kwenye maeneo ya shule katika
kipindi chote cha mtihani. Tukifanya hivyo, tutawawezesha watoto wetu
kufanya mtihani kwa amani na utulivu,” alisema.
Dk. Msonde aliwataka wanafunzi, walimu na wananchi wote kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu wa mtihani huo.
Alisema
baraza halitasita kuchukua hatua kwa yoyote atakayejihusisha na
udanganyifu katika mitihani kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za
utumishi wa umma.
Aidha,
aliwaomba wadau wote kutoa taarifa katika vyombo husika kila
wanapobaini mtu au kikundi cha watu kujihusisha na udanganyifu wa
mitihani ya aina yoyote.
Kwa mujibu wa Dk. Msonde, jumla ya watahiniwa 427,181 wamesajiliwa kufanya mtihani huo ambao utamalizika Novemba 23, mwaka huu.
Alisema kati ya watahiniwa wa shule ni 368,227 na watahiniwa wa kujitegemea ni 58,954.
“Kati
ya watahiniwa wa shule 368,227 waliosajiliwa, wanaume ni 180,908 sawa
na asilimia 49.13 na wanawake ni 187,319 sawa na asilimia 50.87.
Watahiniwa wenye mahitaji maalum wapo 562 kati yao 372 ni wenye uoni
hafifu, 44 wasioona, 109 wenye ulemavu wa kusikia na 37 ni wenye ulemavu
wa viungo vya mwili,” alisema.

No comments:
Post a Comment